Wahusika wa mauaji ya raia huko Borno wasakwe na washtakiwe- Guterres

21 Agosti 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mauaji ya raia wakati wa ghasia zilizotokea huko jimbo la Borno, Kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa takribani watu 19 waliuawa wakati magaidi wa Boko Haram waliposhambulia Kijiji cha Malairi siku ya Jumapili.

Kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa na serikali ya Nigeria huku akitakia ahueni ya haraka majeruhi.

Ametoa wito kwa wahusika wa shambulio hilo wafikishwe haraka mbele ya vyombo vya sheria.
 
Kupitia taarifa hiyo iliyotolewa leo New York, Marekani, Katibu Mkuu Guterres ameendelea kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya ghasia zinazotokea kwenye ukanda wa bonde la Ziwa Chad unaojumuisha nchi za Cameroon, Chad, Niger na Nigeria.

“Amepongeza harakati za kitaifa na za kikanda za kuleta amani na utulivu kwenye eneo hilo na kushughulikia chanzo cha mzozo huo,” amenukuliwa Katibu Mkuu Guterres kwenye taarifa hiyo akisisitiza wito wake kwa jamii ya kimataifa kuongeza usaidizi wake kwa juhudi za kikanda za kukabiliana na kikundi cha Boko Haram katika ukanda huo.

Kwa takribani muongo mmoja sasa magaidi wa Boko Haram wamekuwa wakitekeleza mashambulizi yao kwenye vijiji na kuua raia, kuwateka na kuharibu mali  zao kwenye eneo la kaskazini-mashariki mwa Nigeria na nchi jirani. 

Halikadhalika wamekuwa wakilazimisha watu wanaowateka nyara wajiunge nao ili washiriki kwenye mashambulio ya kujilipua.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter