Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya changamoto Somalia kuna nuru usawa wa jinsia- Phumzile

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN-Women,Phumzile Mlambo-Ngcuka,(kushoto) akiwa na wanawake mjini Baidoa Somalia.
UN Women/Patterson Siema
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN-Women,Phumzile Mlambo-Ngcuka,(kushoto) akiwa na wanawake mjini Baidoa Somalia.

Licha ya changamoto Somalia kuna nuru usawa wa jinsia- Phumzile

Wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN-Women Phumzile Mlambo-Ngucka ameonyesha kutiwa moyo na harakati za ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika mifumo ya kisiasa na michakato yake akisihi hatua zaidi zichukuliwe kuongeza uwakilishi huo.
 

Akizungumza mwishoni mwa juma huko Baidoa mji mkuu wa muda wa jimbo la Kusini-Magharibi la Somalia, Bi. Phumzile-Ngucka amesema bila shaka kuna changamoto kwa wananchi wa Somalia, hususan wanawake na wasichana lakini “kuna fursa kwa mataifa na hizo hutokea mara moja katika kizazi.”

Kwa mantiki hiyo amesema ziara y ake ni kuimarisha  ushirikiano na serikali kuu ya Somalia na kuwatakia kila la kheri katika safari ngumu yenye matumaini ya kujenga upya nchi yao.

Akiwa Baidoa, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UN-Women alikutana na viongozi mbalimbali wakiwemo wajumbe wanawake wa bunge la jimbo hilo pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Somalia inatarajiwa kuwa na uchaguzi mkuu wa mtu mmoja kura mmoja mwaka 2020 ambapo kuelekea uchaguzi wa aina hiyo wa mara ya kwanza, nchi hiyo inatathmini mchakato wa kikatiba ili kubaini masuala kadhaa ikiwemo mgawanyo wa mapato kati ya serikali kuu na zile za majimbo, sambamba na rasilimali pamoja na dhima ya mji mkuu Mogadishu.

Kutokana na hilo, Yasin ambaye ni Waziri wa Jinsia akizungumza wakati wa ziara hiyo amesema watatumia mchakato huo wa mapitio ya katiba kuhakikisha katiba ijayo ya Somalia ina vipengele vinavyopatia wanawake fursa mahsusi ili hatimaye wasichana na wanawake wanufaike siku za usoni.