Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yahitaji dola milioni 11 kusaidia huduma za afya Syria

Msichana akiwa amebeba magudulia ya maji akipita karibu na rundo la taka, katika barabara moja mjini Aleppo, Syria.
UNICEF/Alessio Romenzi
Msichana akiwa amebeba magudulia ya maji akipita karibu na rundo la taka, katika barabara moja mjini Aleppo, Syria.

WHO yahitaji dola milioni 11 kusaidia huduma za afya Syria

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Afya duniani WHO linasaka dola milioni 11 ili kukidhi mahitaji ya huduma za afya kwa wakimbizi wa ndani  walioko majimbo ya Aleppo, Hama, Idleb na Lattakia, kaskazini-magharibi mwa Syria ambako mapigano yanazidi  kupamba moto.

Dk, Michel Thieren ambaye ni mkurugenzi wa kanda wa WHO, anayehusika na masuala ya dharura amesema, “Hali ya afya kwa wakimbizi hao wa ndani walioko  kaskazini magharibi mwa Syria inazidi kuzorora. Ikiwa WHO haitapata fedha za ziada, maisha ya zaidi ya watu  milioni mbili walionasa kwenye mapigano yatakuwa njiapanda na  huenda wakashindwa kupata huduma muhimu za afya, ikiwa ni pamoja na huduma kwa wagonjwa mahututi.”

Pia ameongeza kuwa zaidi ya nusu ya vituo vya afya nchini Syria  vimeshambuliwa au vimelazmilika kufungwa kutokana na migogoro ya kivita inayoendelea  na kwamba wakimbizi wengi wa  ndani wanaishi katika  kambi za muda zilizojaa kupindukia bila huduma za afya, maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi.

 

 

Mvulana huyu akipita maeneo yaliyoharibiwa kufuatia mashambulizi nchini Syria.
© UNICEF/UNI150195/Diffidenti
Mvulana huyu akipita maeneo yaliyoharibiwa kufuatia mashambulizi nchini Syria.

Mkurugenzi huyo amesema kitendo cha wananchi  hao kukosa huduma bora za afya kwa miaka mingi kutokana na mapigano, kinafanya wawe hatarini zaidi kuambukizwa magonjwa. Halikadhalika viwango vya utapiamlo vimeongezeka na kupungua kwa kiwango cha utoaji chanjo kunaweza kusababisha kuibuka kwa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile polio.

Dk. Thieren amesema  tatizo la kukabiliwa na mahitaji mengi katika sehemu nyingi za Syria, watoa huduma za kibinadamu wanajikuta wanaathirika kiutendaji wakati huu ambapo pengo la fedha kwa ajili ya afya limeweka mamilioni ya wasyria kwenye hatari kubwa.

WHO itatumia fedha yoyote ya ziada kutoka kwa wahisani ili kusaidia huduma za afya ya msingi, chanjo kwa watoto na huduma kwa wagonjwa mahututi kaskazini magharibi mwa Syria.

 

Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016
UNICEF
Mtoto akiwa ameketi kwenye dawati ndani ya moja ya darasa la shule iliyoshambulia huko Idleb nchini Syria mwaka 2016

Halikadhalika amesema shirika hilo litatumia fedha hizo kuimarisha mifumo ya kuhamishia wagonjwa hospitali nyingine kwa tiba zaidi il ikuhakikisha wagonjwa walio hoi na majeruhi wanahamishiwa hospitali za huduma maalumu .

Sambamba na hilo WHO itasaidia huduma ya kuhamisha wagonjwa wanaohitaji matibabu pamoja na kliniki na timu ya watoa huduma watakaoweza kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kusaidia kutibu wagonjwa wenye mahitaji.