Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kofi Annan amefariki dunia

Hayati  Kofi Annan
UN /Jean-Marc Ferré
Hayati Kofi Annan

Kofi Annan amefariki dunia

Masuala ya UM

Kofi Annan, raia wa Ghana na Katibu Mkuu wa 7 wa Umoja wa Mataifa ameaga dunia leo.

Kofi Annan amefariki dunia leo akiwa na  umri wa miaka 80.

Annan ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa 7 wa Umoja wa Mataifa kuanzia 1997-2006 amefariki dunia nchini Uswisi baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kupitia mtandao wa Twitter wa taasisi yake #KofiFoundation, imeelezwa kuwa mkewe Nane, na watoto wao Nina, Kojo na Ama walikuwepo wakati mauti yanamfika mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel.

Kufuatia taarifa za kifo chake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea kushtushwa kwake akisema hayati Annan alikuwa msingi thabiti wa uongozi kwa mambo mema.

“Alipanda vyeo kutoka ngazi ya chini kabisa ya Umoja wa Mataifa hadi kuongoza chombo hicho kwenye zama mpya kwa utu na azma isiyo na mfano,” amesema Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake hii leo jijini New  York, Marekani.

Kofi Annan(Katikati) na Mkewe Nane Annan, walipotembelea kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini mwezi Machi mwaka 2006, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
UN/Eskinder Debebe
Kofi Annan(Katikati) na Mkewe Nane Annan, walipotembelea kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini mwezi Machi mwaka 2006, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

GUTERRES NA KOFI

Bwana Guterres amesema, “kama ilivyo kwa wengi, nilikuwa najivunia kumuita Kofi Annan rafiki mwema na kiongozi kwa kunilea kimajukumu. Ilikuwa ni heshima kubwa kwangu kwa yeye kuniamini na kunichagua kuwa Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, chini ya uongozi wake.”

Kwa mujibu wa Guterres ,  hayati Annan alisalia kwa mtu ambaye alimfuata kwa ajili ya ushauri na busara, akisema kuwa “naamini siko peke yangu. Aliwapatia watu popote pale alipo fursa ya mazungumzo, fursa ya kutatua matatizo na mwelekeo wa kuwa na dunia bora zaidi.”

Bwana Guterres amesema katika zama za sasa za misukosuko na majaribu, “katu hakuchoka kufanya kazi na kupatia uhai misingi ya katiba ya Umoja wa Mataifa. Mchango wake utasalia hamasa kwetu sote.”

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya hayati Annan na wale wote wanaoomboleza kifo cha mwendazake huyo aliyekuwa bingwa halisi wa dunia wa amani na utu.

AMINA J. MOHAMMED

Kufuatia kifo hicho ha Kifo Annan, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J,. Mohammed  amesema hayati Annan alishi maisha ambayo kila wakati alijitolea kuhudumia utu wa kibinadamu. "Alitekeleza jukumu hilo kwa utu  na akapatiwa matumaini wasiokuwa na sauti. Rafiki yangu, Shujaa wangu, na mtu aliyenipatia hamasa," amesema Bi. Mohammed kupitia mtandao wake wa Twitter.

Tweet URL

ZEID AMZUNGUMZIA KOFI ANNAN

Kwaheri rafiki yangu Kofi! Ndivyo inavyosema taarifa ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein iliyotolewa punde tu baada ya ripoti za kifo cha Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo imechapishwa katika mtandao wa Facebook wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR.

Bwana Zeid amesema “nimehuzunishwa sana na taarifa hizi za kuaga dunia kwa Kofi Annan.. Kofi alikuwa alama bora zaidi ya ubinadamu, utu na neema. Katika dunia iliyojaa viongozi wachache kama yeye, kuondoka kwake kunakuwa na machungu zaidi.” Ameongeza kuwa alikuwa rafiki kwa maelfu na kiongozi kwa mamilioni

Kamishna Zeid amesema kwake yeye, na kama ilivyo kwa wengi “alikuwa kiongozi wangu wakati nina  umri wa miaka 30. Kiongozi wa aina yake. Kila wakati alikuwa jasiri, aliongea kilicho moyoni na katu hakukuvunjia heshima,katu. Baadaye nilipokuwa Balozi Umoja wa Mataifa alikuwa kichocheo kwetu, kwa kuwa kiongozi mwenye mvuto akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.”

Wakati huo huo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajcak katika ujumbe wake ameelezea masikitiko na majonzi yake kufuatia kifo cha Annan.

Amesema “”Kofi Annan mmoja wa washindi wa tuzo ya amani ya Nobel “alikuwa mtu wa amani na mlinzi wa amani, maendeleo pamoja na haki za binadamu.Alitoa uhai wake wote  kuona ulimwengu unakuwa sawa, wenye amani zaidi na nafasi kwa watu wote.”