Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za Ebola kwa watoto DRC ni zaidi ya kuugua -UNICEF

UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.
WHO/Lindsay Mackenzie
UNICEF inasema watoto wameathirika mno na mlipuko wa Ebola mashariki mwa DRC.

Athari za Ebola kwa watoto DRC ni zaidi ya kuugua -UNICEF

Afya

Watoto wanawakilisha idadi kubwa isiyo ya kawaida ya waathirika wa mlipuko wa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, limesema shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF

Katika taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo  kwa wakati mmoja katika miji tofauti ya New York Marekani, Geneva Uswisi, Kinshasa, DRC na pia Dakar Senegal, hadi sasa watoto wawili wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Halikadhalika vituo vya kutibu wagonjwa wa Ebola katika miji ya Beni na Mangani kwenye jimbo la Kivu Kaskazini vinapatia matibabu watoto sita ambao wameambukizwa au wanashukiwa kuwa na Ebola.

UNICEF imeorodhesha watoto 53 ambao sasa ni mayatima baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Watoto wakiwa nje ya kambi ya  watu wasio na makazi katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Photo: UNHCR/B. Sokol
Watoto wakiwa nje ya kambi ya watu wasio na makazi katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Dkt. Gianfranco Rotigliano, anasema kuwa watoto ambao wameathiriwa na mlipuko wa Ebola wanahitaji  sio tu huduma maalum lakini pia kutunzwa.

Ameongeza kuwa wanawake kimsingi ndio walezi wa kwanza wa  watoto, kwa hivyo ikiwa wameambukizwa ugonjwa huo kuna hatari kubwa ya kuambukiza watoto na familia zao.

 Shirika hilo likiwa na wadau wake limetoa mafunzo kwa washauri nasaha 88ambao watasaidia na kuwafariji watoto katika vituo mbalimbali na wale watoto ambao wameshatibiwa na kutoka vituoni lakini huenda wakasumbuliwa na unyanyapaa.

Dkt. Rotigliano ameongeza kuwa athari za ugonjwa huo kwa watoto sio tu kwa wale walioambukizwa au wanaoshukiwa kuwa waliambikizwa.

Badala yake amesema watoto wengi wanakabiliwa na  magonjwa au vifo vya wazazi au wapendwa wao huku watoto wengine wamewapoteza familia nzima  na wamebaki peke yao na hivyo amesema watoto hao wanahitaji msaada.

Amesema hivi sasa shirika hilo linasaka na kusidia familia za kupokea na kutunza watoto hao na pia inawapatia huduma za ushauri nasaha na chakula.