Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maji yakiwa jirani watoto wana muda wa kusoma na kucheza

Picha ya watoto wakicheza kwenye bomba la maji, mradi wa UNICEF wa kuwawezesha wakimbizi kupata maji.
UNICEF/UN055929/Gilbertson VI
Picha ya watoto wakicheza kwenye bomba la maji, mradi wa UNICEF wa kuwawezesha wakimbizi kupata maji.

Maji yakiwa jirani watoto wana muda wa kusoma na kucheza

Msaada wa Kibinadamu

Suluba ya kutembea muda mrefu wakati akiwa mtoto ili kutafuta maji ilikuwa ni kichocheo kwa kijana mmoja huko Sudan Kusini kuamua kusoma uhandisi na sasa amefanikisha kujengea jamii yake mfumo endelevu wa maji safi na salama.

Kijana huyo Josaphat Kambale akizungumza kwenye video ya kampeni ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, iliyopatiwa jina Maji safi kwa kila mtoto, amesema akiwa na umri wa miaka sita alilazimika kuamka saa tisa alfajiri kwenda kusaka maji na alirejea nyumbani saa moja asubuhi.

Sauti ya Josaphat Kambale

“Nilpofikisha umri wa miaka 16 walijenga kisima karibu na nyumbani, na hiyo kwangu ilikuwa ni furaha kubwa sana. Baada ya hapo nilishawishika sana kujifunza mbinu za uchimbaji visima, ujenzi wa mabomba ya maji  ili   kuhakikisha kwamba watoto kama mimi wakati huo wana maji karibu na nyumbani kwao na wanaweza kwenda shule.”

Na hatua hiyo ilileta msukumo kwa Bwana Kambale..

Sauti ya Josaphat Kambale

“Hiyo ilinipa msukumo wa kwenda katika chuo cha uhandisi, ili nielewe ni kwa jinsi gani  maji yanaweza kutoka mahali yalipo na kuwafikia watoto”.

Hivi sasa Bwana Kambale ni injinia wa mradi wa huduma za kujisafi wa UNICEF uitwao WASH na ana furaha kwa kuwa ..

Sauti ya Josaphat Kambale

“Nikiona maji katika jamii mbalimbali, najihisi mwenye furaha sana. Nafikiri watoto wana furaha sana kwasababu maji yakiwa jirani wanatumia muda mchache kuchota na mzigo umepunguzwa kwao na wana muda wa kucheza.”