Wafanyakazi wanaosafisha mtambo wa Fukushima Daiichi wanadhulumiwa
Japan ichukue hatua haraka kulinda makumi ya maelfu ya wafanyakazi wanaoripotiwa kudhulumiwawakati wanafanya kazi ya kusafisha mtambo wa nyuklia ulioharibika wa Fukushima Daichi.
Hayo yamesemwa na wataalamu watatu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi hii leo, wakisema kuwa wafanyakazi hao wanakabiliana na minururisho ya nyuklia yenye sumu.
Wataalam hao wamesema wafanyakazi hao walioajiriwa kusafisha mtambo huo wa Fukushima Daiichi ni wahamiaji, wasaka-hifadhi pamoja na watu wasio na makazi.
Hofu yao wataalamu hao ni kwamba wafanyakazi hao wanaweza kuwa wamehadaiwa juu ya hatari zitokanazo na minururisho wakati wa kusafisha mtambo huo, wameshinikizwa kukubali kufanya kazi katika mazingira hatari kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili au hawana mafunzo ya kujikinga.
Na zaidi ya yote wanasema “ripoti za kina zinaonyesha kuwa kandarasi ya kuondoa sumu kwenye eneo la mtambo zilipatiwa wakandarasi wakubwa na kwamba kampuni mamia ya kampuni ndogo yasiyo na uzoefu yalipatiwa kandarasi ndogo za kusaka watu wa kufanya kazi hiyo kupitia madalali, hali ambayo inaweza kuwa iliweka mazingira bora ya kudhulumu wafanyakazi na kukiuka haki zao.”
Kwa kuzingatia hilo, wataalamu hao wana hofu juu ya madhara ya minururisho hiyo kwa afya za mwili na akili za wafanyakazi hao.
Uchafuzi wa eneo hilo na kuenea kwa minururisho ya nyuklia vinasalia kuwa ni hatari kubwa kwa wafanyakazi wanaojaribu kulifanya liwe salama tena, miaka saba baada ya mtambo huo kusambaratikakutokana na tetemeko la ardhi lililofuatiwa na tsunami.
Kwa kipindi cha miaka saba sasa, mamia ya maelfu ya wafanyakazi wameajiriwa ili kusafisha eneo hilo chini ya mpango maalum wa kuondoa sumu hiyo.
Katika wavuti wake wizara ya Afya, Kazi na Maslahi nchini Japan inaonyesha kuwa wafanyakazi 46,386 waliajiriwa mwaka 2016, huku kituo cha kusajili wafanyakazi wahusikao na masuala ya minururisho nchini humo kilionyesha kuwa kiliajiri watumishi 76,951 katika kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2016.