Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutaheshimu uamuzi wa wakimbizi kuhusu kurejea nyumbani- Tanzania

Mkimbizi kutoka Burundi anayeishi kwenye kambi ya Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania .
UNHCR/Benjamin Loyseau
Mkimbizi kutoka Burundi anayeishi kwenye kambi ya Nduta mkoani Kigoma nchini Tanzania .

Tutaheshimu uamuzi wa wakimbizi kuhusu kurejea nyumbani- Tanzania

Wahamiaji na Wakimbizi

Naibu Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Volker Turk amehitimisha ziara yake  ya siku nne nchini Tanzania akisisitiza umuhimu wa wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa jijini Dar es salaam, mwishoni mwa ziara hiyo imemnukuu Bwana Turk akisisitiza uhuru wa wakimbizi kuchagua iwapo wanataka kurejea nyumbani au la na wafanye hivyo wakiwa na taarifa sahihi na bila shinikizo lolote.

“Wakimbizi wanahitaji uamuzi sahihi kuhusu iwapo wanataka kurejea au la kwa kuzingatia hali halisi ilivyo kule wanakorejea. Hakapaswi kuwepo na shinikizo la moja kwa moja au lisilo la moja kwa moja katika kutekeleza suala la wakimbizi kuchagua kurejea nyumbani,” amesema Bwana Turk baada ya ziara hiyo iliyomkutanisha pia na wakimbizi kwenye kambi ya Nduta mkoani Kigoma.

Akiwa Kigoma alishuhudia wakimbizi wakirejea nyumbani Burundi kwa hiari ambapo mpaka sasa wakimbizi zaidi ya 42,000 wamerejea nyumbani.

 

Naibu Kamishna Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa akizungumza na wakimbizi wakati wa ziara yake kwenye kambi  ya wakimbizi ya Nduta mkoani Kigoma.
UNHCR Tanzania/Abdul Khalif
Naibu Kamishna Mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa akizungumza na wakimbizi wakati wa ziara yake kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta mkoani Kigoma.

Kwa upande wake, serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya UNHCR, imehakikishia shirika hilo kuwa uamuzi wa wakimbizi kurejea au kutorejea utaheshimiwa.

Kuhusu hali ya Burundi, Naibu Kamishna Turk alikuwa na mkutano na viongozi wa kikanda wa UNHCR kutoka nchi ambazo zinahifadhi wakimbizi kutoka nchi hiyo ya  ukanda wa Maziwa Makuu.

Msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi wa Burundi bado hautoshelezi ambapo UNHCR na wadau wake wamepokea asilimia 12 tu ya dola milioni 391 zilizoombwa kwa mwaka huu wa 2018.

Kwa mantiki hiyo Bwana Turk ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuangazia eneo hilo ili kufanikisha mahitaji kwa wakimbizi.