Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Atakayetumia JUJU kufanikisha usafirishaji haramu kukiona cha mtema kuni

Hali ilivyo katika maeneo ya kushikilia wahamiaji na wasaka hifadhi. Hapa ni Libya nje kidogo ya mji mkuu, Tripoli.
UNICEF/Alessio Romenzi
Hali ilivyo katika maeneo ya kushikilia wahamiaji na wasaka hifadhi. Hapa ni Libya nje kidogo ya mji mkuu, Tripoli.

Atakayetumia JUJU kufanikisha usafirishaji haramu kukiona cha mtema kuni

Wahamiaji na Wakimbizi

Kufuatia kitendo cha baadhi ya wasafirishaji  haramu wa binadamu huko Afrika Magharibi, kudaiwa kutumia nguvu za giza au JUJU kama tishio kwa wale wanaosafirishwa, shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limekutana na msemaji wa chifu mmoja ambaye amechukua hatua kuondokana na fikra hizo potofu.

Nats…

Huyu ni Chifu Sam Igbe Iyase wa Benin, moja ya nchi ambako ni njia ya asilimia 94 ya wanawake wa Nigeria wanaosafirishwa kiharamu, hapa anakutana na  maafisa wa IOM

Chifu Igbe ambaye ni msemaji wa kabila la Oba nchini humo anaweka bayana kuwa idadi kubwa ya wasafirishaji  haramu wa binadamu hulaghai watu kuwa ili safari yao ya kwenda kusaka maisha bora Ulaya iwe salama na mafanikio ni lazima walipe kiasi cha fedha kwa waganga wa jadi na wabebe kinga au JUJU.

(Sauti ya Chifu Igbe)

“Ni kwa ajili ya kuwajengea hofu. Kwa hiyo wakifika huko wanaendelea kulipa fedha tena wakati mwingine kiasi kikubwa kuliko walichoahidi nyumbani, lakini wanalipa wakiamini kuwa JUJU itawaua iwapo hawatalipa.”

Hata hivyo amesema baada ya  kubaini hilo ni tatizo kubwa na kutambua kuwa JUJU yoyote haiwezi kufanya kazi iwapo  Oba ambaye ni mtawala wa kabila la Yoruba atasema hapana..

(Sauti ya Chifu Igbe)

“Oba aliamua kuweka wazi kwa kila mtu, iwe wasafirishaji au wasafirishwaji, na familia zao kuwa hiki kitu lazima kikome, vitisho vya juju vikome na visipokoma yeyote anayehusika navyo atajilaumu mwenyewe. Popote pale ulipo, Benin, Uingereza, Lagos au Abuja, Oba anasema hiki ndio kitakupata iwapo hutaacha.”

Msemaji huyo amesihi watu kusaka mbinu sahihi za kuingia ugenini badala ya kupitia njia zisizo rasmi.