Ushirikiano wa kimataifa unasalia muarobaini wa changamoto duniani

14 Agosti 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa ripoti yake ya mwaka inayoweka bayana juu ya umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kutatua changamoto zinazokabili ulimwengu hivi sasa.

Ikipatiwa jina la ripoti ya Katibu Mkuu juu ya kazi ya shirika kwa mwaka 2018, ripoti inamulika maeneo muhimu ambayo Umoja wa Mataifa unaangazia ambayo ni amani na usalama, maendeleo, misaada ya kibinadamu na maendeleo.

Katibu Mkuu ameweka bayana kuwa changamoto kama amani ambayo aliipatia kipaumbele wakati anaanza kutumikia Umoja wa Mataifa mwaka 2017, bado ipo akisema kuwa mizozo imezidi kushika kasi, haki za binadamu zinasiginwa, ukosefu wa usawa umeshamiri huku ubaguzi dhidi ya wanawake ukisalia ni tatizo.

 

UNHCR/Bassam Diab
Mama mkimbizi wa Syria aliyekimbia mapigano makali katika mji wa Ghouta anachemsha mayai akitumia makatarasi magumu kama kuni.

 

AJENDA 2030

Katika moja ya sura pili ya ripoti hiyo  yenye kurasa 76, Katibu Mkuu anaangazia utekeleza wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs akisema bado kuna tofauti kubwa katika kufanikisha malengo  hayo.

Mathalani mwaka 2015, watu watatu kati ya 10 ulimwenguni hawakuwa na uwezo wa kupata maji safi na salama, na asilimia 60 hawakuwa na huduma za kujisafi. Zaidi ya yote majangana mabadiliko ya tabianchi yanaathiri wakazi wa dunia.

Hata hivyo amepongeza mapitio ya hiari ya nchi wanachama kuhusu utekelezaji wa malengo hayo akisema, “yametoa fursa kwa nchi kutambua kile ambacho wenzao wanafanya na hivyo kujiweka katika mwelekeo sahihi wa kuyatekeleza.”

Katibu Mkuu amesema umoja na ujasiri vinahitajika ili kufanikisha ajenda hiyo yenye malengo 17 na hatimaye kutokomeza umaskini na kujenga jamii tulivu, zenye amani na ustawi.

PICHA: UN /Manuel Elias
Katibu Mkuu wa UM Antonio Guterres akiwa na Mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, AU Moussa Faki Mahamat kwenye mkutano na wanahabari jijini New York Marekani.

USHIRIKIANO NA AFRIKA

Suala la ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na bara la Afrika kupigia Muungano wa Afrika, AU limepatiwa pia kipaumbele kwenye ripoti hiyo ambapo Katibu Mkuu amesema unazingatia kuheshimiana, mshikamano na kusaidiana.

Bwana Guterres amesema “Umoja wa Mataifa mwaka huu wa 2018 umetekeleza shughuli kadhaa kwenye nchi kadhaa za Afrika, mfano Angola, Burkina Faso, Cameroon, Comoro,  Gambia, GuineaBissau, Madagascar, Mali na Tanzania ambapo tumewapatia mifumo jumuishi na program zilizoundwa na tume ya uchumi ya UN kwa Afrika ili kuoanisha malengo madogo ya SDGS na ajenda 2030.”

 

MAREKEBISHO YA KIMUUNDO

Katibu Mkuu Guterres amezungumzia pia marekebisho ya kimuundo yaliyoanza kwenye chombo hicho kilichoundwa mwaka 1945, marekebisho yanayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Amina Mohammed ili kuimarisha utendaji wake na pia kuwa na mashiko mashinani.

UNAMID/Hamid Abdul Salaam
Vijana wakiwa kwenye mkutano huko El Fasher, Darfur, Sudan.

UJUMUISHAJI VIJANA

Ripoti pia imegusia vijana na hatua zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa kutetea na kuhakikisha vijana wanajumuishwa kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi.

Kwa mantiki hiyo amesema “kwa kutambua umuhimu wa vijana na changamoto tunazokabiliana nazo katika kutumia uwezo wao na kushughulikia shaka zao, Umoja wa Mataifa umepitisha mkakati wake kuhusu vijana. Kupitia mkakati huu, tunasaka kuimarisha ushirikiano wetu na vijana katika misingi yote ya amani, usalama, maendeleo endelevu na usaidizi wa kibinadamu.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud