Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde wapiganaji DRC wekeni silaha chini ili tukabili Ebola- WHO

Walinda amani wa MONUSCO wasema wako tayari kuimarisha usalama kwenye harakati za kukabiliana na Ebola.
MONUSCO
Walinda amani wa MONUSCO wasema wako tayari kuimarisha usalama kwenye harakati za kukabiliana na Ebola.

Chonde chonde wapiganaji DRC wekeni silaha chini ili tukabili Ebola- WHO

Afya

Shirika la afya duniani, WHO limetoa wito kwa vikundi vilivyojihami huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC viweke silaha chini ili kama njia mojawapo ya kufanikisha harakati za kuepusha kuenea zaidi kwa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ahanom Ghebreyesus, amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Geneva, Uswisi baada ya ziara yake mwishoni mwa wiki kweny mji wa Beni huko DRC ambako ni kitovu cha mlipuko wa Ebola.

Amesema ana hofu kubwa na mlipuko wa sasa kuliko mlipuko wa hivi karibuni uliotokea takribani maili 2,500 magharibi mwa DRC kutokana na hali duni ya  usalama inayokwamisha operesheni dhidi ya Ebola.

“Tangu mwezi Januari kumekuwepona matukio 120 ya mapigao makali; kama hiyo haitoshi, usiku ambao tulikuwepo mjini Beni, kulikuwepo na mapigaon ndani ya kilometa mbili na raia wanne waliuawa, wengine wengi walitekwa, kwa hiyo mazingira ni rafiki kwa Ebola kuenea kwa urahisi.”

Hadi sasa watu 41 wamefariki dunia kutokana na Ebola kwenye jimbo la Kivu Kaskazini tangu ugonjwa huo uripotiwa mwanzoni mwa mwezi huu.

Licha ya changamoto za usalama na kushindwa kuwafikia watu wanaohofiwa kuambukizwa ugonjwa huo, Dkt. Tedros amesema harakati za kukabili Ebola zinakwamishwa pia na muingiliano mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya mipaka ya DRC.

Hata hivyo amesema anatumai kuwa iwapo watapata rasilimali za kutosha, mlipuko huo unaweza kuwa umedhibitiwa ifikapo mwezi disemba, wakati ambapo DRC itakuwa inafanya uchaguzi wa rais.