Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Paraguay kwa kuchukua hatua kulinda wasio na utaifa

Mtu asiye na makazi katika mitaa ya Asunción, Paraguay.
UN/Rocío Franco
Mtu asiye na makazi katika mitaa ya Asunción, Paraguay.

Heko Paraguay kwa kuchukua hatua kulinda wasio na utaifa

Wahamiaji na Wakimbizi

Umoja wa Mataifa umekaribisha hatua ya Paraguay ya kupitisha sheria mpya inayosaidia kutambua, kulinda na kupatia suluhu ya kudumu suala la ukosefu wa utaifa kwa baadhi ya wananchi wanaotambuliwa kutokuwa raia nchini hum

Sheria hiyo ilipitishwa na Baraza la Congresi Alhamisi iliyopita kufuatia muswada uliowasilishwa mwezi mei mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa  UNHCR William Spindler amesema sheria hiyo inalinda haki za watu wasio na utaifa Paraguay na sasa wanaweza kuwasilisha maombi ya utaifa sambamba na kusaidiwa kupata uraia.

Amesema Tume ya Taifa ya wakimbizi nchini humo, CONARE, imepatiwa jukumu la kusaidia kuhakikisha kuwa watoto wa raia wa Paraguay waliozaliwa nje ya nchi hiyo ambao wangalitambuliwa kuwa hawana utaifa, wapatiwe utaifa bila hata ya kuwa wakazi wa nchi hiyo.

 Kwa mujibu wa Spindler, sheria hiyo ni muhimu na ni ya kihistoria kwa ukanda wa Amerika ya Kusini, eneo ambalo amesema linahaha kuondokana na wananchi kukosa utaifa, na ni hatua inayoendana na ahadi zilizotolewa na nchi hizo mwaka 2014 nchini Brazil.

Mwaka 2014, UNHCR ilizindua kampeni ya #IBelong au #Miminiwa ikilenga kuondokana na kitendo cha watu kutokuwa na utaifa ifikapo mwaka 2024.

Kupitia kampeni hiyo, UNHCR inalenga kuimarisha hatua za serikali na mashirika ya kiraia kusaka haki za watu hao ambao wananyimwa haki zao za msingi kama vile elimu, afya, ajira, kuolewa, kuoa, kusafiri  na hata kufungua akaunti za benki.

UNHCR inasema mwaka 2012, Paraguay iliridhia mkataba wa kimataifa wa kuondokana na ukosefu wa utaifa wa mwaka 1961 na mwaka 2014, iliridhia mkataba mwingine unaohusiana na watu wasio na utaifa.

 

TAGS: UNHCR, Paraguay, IBelong