Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanamgambo wafurusha wakimbizi Libya, UNHCR yapaza sauti

Msichana mdogo aliyefurushwa akicheza nje ya makazi yao mapya huko Benghazi, ambapo palikuwa ni jengo la  kampuni.
UNHCR/ L. Dobbs
Msichana mdogo aliyefurushwa akicheza nje ya makazi yao mapya huko Benghazi, ambapo palikuwa ni jengo la kampuni.

Wanamgambo wafurusha wakimbizi Libya, UNHCR yapaza sauti

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR lina wasiwasi na hatua iliyochukuliwa na wanamgambo huko nchini Libya ya kuwafurusha wakimbizi wa ndani 1900 kutoka makazi yao huko Triq Al Matar, mjini Tripoli.

Msemaji wa UNHCR huko Geneva, Uswisi, William Spindler amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa makazi hayo ndio makazi makubwa zaidi kwa wakimbizi wa ndani mjini  humo yakihifadhi tangu mwaka 2011 familia 360 za kabila dogo kutoka mji wa Tawergha.

Amenukuu wakazi hao wakisema kuwa walifurushwa baada ya siku tatu za vitendo vya wanamgambo hao kuvamia eneo hilo na kukamata watu 94, ambapo 12 kati  yao hadi sasa wanashikiliwa katika mazingira mabaya.

Amesema baadhi yao ni wanawake na wasichana ambao walitishiwa kubakwa na hivyo kulazimika kukimbia na virago vichache kwenda kusaka hifadhi kwa jamaa zao.

(Sauti ya William Spindler)

“UNHCR ina wasiwasi kuwa wakimbizi hao licha ya kukimbilia maeneo mengine huko Tripoli, bado wataweza kufurushwa tena. Baadhi ya familia kutoka Tawerga zinazoishi kwenye makazi mengine zina hofu ya kushambuliwa na wameshakimbia makazi yao. UNHCR inatoa wito wa kuheshimu haki za binadamuna kulinda raia na pia haki za wakimbizi kuamua mustakhbali wao.

Idadi kubwa ya watu hao kutoka mji wa Tawerga wamekuwa wakiishi kwenye makazi  yasiyo rasmi huko Tripoli au Benghazi wakiwa wakimbizi wa ndani kwa miaka 7 sasa.

Hivi sasa wanasubiri kurejea nyumbani kufuatia makubaliano ya hivi karibuni kati ya pande husika kwenye mzozo.

UNHCR inatoa wito kwa suluhu ya haraka ili waweze kurejea nyumbani kwa hiari na kwa njia ya kiutu na salama.

 

Tweet URL