Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machungu ya raia ndio kichocheo changu cha kupaza sauti- Zeid

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein wakati wa ziara yake huko Tripoli, Libya tarehe 10 Oktoba 2017
UNSMIL/Abel Kavanagh

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema machungu wanayopitia wahanga wa ukiukwaji wa haki  za binadamu ni shinikizo kubwa kwake yeye kuzungumza bila woga.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini ya awamu yake ya miaka minne wakati huu anapomaliza jukumu hilo Bwana Zeid amesema.

(Sauti ya Zeid Ra’ad Al Hussein)

“Shinikizo kubwa kwenye kazi yetu hutoka kwa waathirika na wale walioko kwenye machungu ambao wana matarajio makubwa kutoka kwetu. Na hilo ndilo shinikizo ambalo ni muhimu zaidi na lina athari kubwa kwetu hasa katika kufanya jambo sahihi.”

Kamishna Zeid akatoa mfano wa kisa kimoja akisema kuwa “nilikutana na wasichana wanne. Walikuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela- kwa kuwa na wakidai hii ilitokana na dharura ya kiukunga, hizo zilikuwa ni mimba zilizotoka bahati mbaya – serikali ilidai kuwa mimba zilizotolewa makusudi.”

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra'ad Al Hussein (kushoto) akiwa  katika moja ya ziara zake. Hapa ni DRC akiwa ameambatana na Dkt. Denix Mukwege, bingwa wa kutibu wanawake waliokumbwa na ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji
MONUSCO

Amesema alipozungumza nao alikuwa na timu yake yote na kwamba anadhani ndani ya takribani dakika 10 za mazungumzo hayo wote walikuwa wanalia, walitokwa na machozi kwasababu machungu ya wasichana hao yalikuwa ya kupindukia.

Bwana Zeid akasema kwa kuzingatia jukumu la kamishna mkuu wa haki za binadamu la kutetea waathirika, msimamo wa kupaza sauti ni wajibu hivyo akasema kwamba “siamini kama mtu anayeshika nafasi hii, hata kama atakuwa na mtazamo tofauti, anaweza kutekeleza majukumu kwa njia ambayo haitokuwa na msimamo mkali kama nilivyofanya mimi na watangulizi wangu.”

Hao nawavulia kofia. Nina maana nitawathamini na nitawakumbuka

Amesema imani  yake ni kwamba iwapo kamishna mkuu atajaribu kwenda pembeni, atasikia tu, na itakuwa si vyema kwake kwasababu atasikia kilio hicho kutoka kwa watu ambao wanakabiliwa na machungu.

Kuhusu makundi ambayo alipenda kufanya nayo kazi zaidi, Kamishna Zeid ambaye ni raia wa Jordan ameyataja kuwa ni mashirika ya kiraia, makundi ya waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu na watetezi wa haki za binadamu ambao wako chini ya ofisi yake.

Bwana Zeid amesema iwapo makundi hayo yatasema kuwa yeye alifanya kazi nzuri basi atafurahi sana na iwapo wakisema kuwa angaliongeza juhudi zaidi,basi atakubali hilo na kuishi nalo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein akimsikiliza mmoja wa wanaharakati na muathirika wakati wa ziara  yake Guatemala mwezi Novemab mwaka 2017
OHCHR
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein akimsikiliza mmoja wa wanaharakati na muathirika wakati wa ziara yake Guatemala mwezi Novemab mwaka 2017

Umoja wa Mataifa umekuwa ukikosolewa kwa nyakati tofauti kwa madai ya kutofanya kazi yake ipasavyo kutetea wakazi walio kwenye nchi 193 wanachama wa chombo hicho kilichoanzishwa mwaka 1945. Kamishna Zeid alipoulizwa kwenye mahojiano hayo amesema ni vigumu sana kustahmili udhalilishaji wa Umoja wa Mataifa pindi anapofikiria vitu vya kishujaa vinavyofanywa na watu huko mashinani.

“iwe ni watoa huduma za kibinadamu, au wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, watetezi wa haki za binadamu au watu wanaofuatilia haki. Hao nawavulia kofia. Nina maana nitawathamini na nitawakumbuka,” amehitimisha Kamishna Zeid.

Kamishna  huyu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anahitimisha jukumu lake tarehe 31 mwezi huu wa Agosti na nafasi yake inachukuliwa na Michelle Bachelet kutoka Chile aliyethibitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein akiwa na mkuu wa zamani wa ofisi ya haki za binadamu ya UN huko Colombia, Todd Howland. Hapa alikuwepo ziarani Colombia Septemba 2016