Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN asilani haipaswi kulengwa na magaidi: Manusura

Makao mkuu ya UN Baghdad baada ya shambulio la 19 Agosti 2003
UN Photo/AP Photo
Makao mkuu ya UN Baghdad baada ya shambulio la 19 Agosti 2003

UN asilani haipaswi kulengwa na magaidi: Manusura

Amani na Usalama

Tarehe 19 Agosti 2003, Umoja wa Mataifa ulipata pigo kubwa pale mshambuliaji wa kiujitoa muhanga alipoendesha lori lake ililosheheni vilipuzi hadi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad nchini Iraq na kujilipua. Shambulio hilo katika jengo la Hotel ya Canal lilikatili maisha ya watu 22 miongoni mwao ni Sergio Vieira de Mello, aliyekuwa Kamishina Mkuu wa haki za binadamu na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq.

Watu wengine zaidi ya 150 wengi wao wakiwa wafanyakazi wa misaada waliofika Iraq ili kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo baada ya kuangushwa kwa utawala wa rais Saddam Hussein.

Shambulio hilo lilikuwa moja ya mashambulio mabaya zaidi katika historia ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ni mwanzo wa mabadiliko ya jinsi Umoja wa Mataifa wa wahudumu wa misaada wanavyoendesha shughuli zao mashinani.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa shirika la kimataifa la masuala ya kibinadamu lisiloegemea upande wowote kulengwa maksudi kwa njia hiyo.

 

Baraza la usalama la  Umoja wa Mataifa latafakari hali nchini Iraq
UN Photo/Loey Felipe
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa latafakari hali nchini Iraq

 

wiki hii katika kuelekea kumbukumbu ya miaka 15 tangu kutokea shambulio hilo ambalo“ni moja ya jinamizi kubwa katika historia ya Umoja wa Mataifa UN news imezungumza na baadhi ya manusura ambao wanakumbuka kilichotokea siku hiyo, jinsi walivyoathirika na shambulio hilo linavyoendelea kuaathiri jamii ya Umoja wa Mataifa .

Miongoni mwao ni Andrew Clapham profesa wa sheria Geneva Uswis na alikuwa mshauri wa Bwana.

De Mello, wakati huo alikuwepo Baghadad kwa muda wa wiki chache tu anasimilia ilivyokuwa,“nilihitaji kwenda msalani, na maliwato kwenye ofisi hizo za Umoja wa Mataifa zilikuwa ghorofa ya chini ya ardhi ambako hakuna madirisha, na mlipuko ulipotokea nilikuwa nina bahati sana kwani nilikuwa msalani na hakukuwa na vioo vilivyokuwa vinaruka na kupasuka, na ninachokumbuka ni mlio mkubwa kabisa ambao sijawahi kuusikia maishani  kisha umeme ulizimika na nikawa kwenye giza totoro.”

Nabaada ya hapo?“Na kisha nakumbuka nilikuwa nimekwama kidogo na nikajitahidi kuchoropoka na kuanza kutafuta njia gizani kwenye ngazi na ndipo nikawaona watu wengi waliojeruhiwa vibaya , wakijaribu kutafuta kwenye mwangaza , na ndipo nakumbuka wakatuambia Sergio de Mello ameuawa, kwanza hatukuamini tulidhani ni uzushi tu, na kama ujuavyo kwa bahati mbaya ilikuwa kweli, ilikuwa zahma kwa kila mtu.”