Serikali ya Belarus acheni kukandamiza haki ya kujieleza- Mtaalamu

10 Agosti 2018

Kamatakamata ya kiholela inayolenga wachapishaji huru na waandishi wa habari nchini Belarus ni alama ya sheria mpya za ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vya mtandaoni nchini humo.

Amesema hayo mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya  haki za kibinaadamu  nchini Belarus , Miklos Haraszti.

Kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, mtaalamu huyo amesema “hatua hizi zina lengo la kufuta hali  ya uandishi habari wa kujitegemea nchini Belarus  ili kufuata sheria mpya kandamizi zilizopitishwa mwezi Juni dhidi ya  vyombo huru vya habari vya mtandaoni.”

Ili kudhihirisha hali mbaya huko Belarus, taarifa hiyo inasema kuwa tarehe 7 na 8 mwezi huu wa Agosti,maafisa wa serikali walifanya upekuzi katika ofisi kadhaa na pia kuzuia operesheni za vyombo vya habari mbalimbali ambapo moja wa chombo cha habari kilichofungwa ni mtandao wa Tut.by na  shirika pekee la habari huru nchini humo la BelaPAN.

Duru zinasema kuwa katika kamatakamata hiyo, takriban waandishi habari 18 walibebwa akiwemo  mhariri mkuu wa Tut.by, Maryna Zolataya na zaidi ya yote wafanya kazi wa vyombo hivyo vya habari walizuiliwa kuingia ofisini mwao.  

Yaelezwa kuwa operesheni ya serikali ilichochewa na madai ya ukiukwaji sheria ambazo huwa ni kosa la jinai kupata habari ndani ya kompyuta kupitia njia zisizo halali na ambapo habari hizo zinaweza kusababisha uharibifu.

Kwa mujibu wa sheria mpya, mtu atawajibika endapo ataendesha shughuli zozote za mtandaoni ikiwemo mitandao ya kijamii iwapo hana leseni kutoka serikalini.

Haraszti amesema kunyamazisha vyanzo vya mwisho kabisa ambayo vinawezesha wananchi wa Belarus kutambua hofu ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini humo ni kitu cha ajabu sana kwa kuzingatia kuwa serikali inadai kushirikiana na Umoja wa Mataifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud