Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni mapigano ili kunusuru maisha ya watoto Yemen :UN

Kijana acheza akipita magofu ya nyuma zilizoharibiwa na mashambulio ya angani katika mji wa zamani wa Saada.
N OCHA/Giles Clarke
Kijana acheza akipita magofu ya nyuma zilizoharibiwa na mashambulio ya angani katika mji wa zamani wa Saada.

Sitisheni mapigano ili kunusuru maisha ya watoto Yemen :UN

Amani na Usalama

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa  Mataifa, OHCHR pamoja  na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wametoa wito kwa pande kinzani katika migogoro ya kivita inayoendelea nchini Yemen kusitisha mapigano ili kuokoa maisha ya raia wasiokuwa na hatiawakiwemo na watoto .

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, Liz Throssel ambaye ni msemaji wa OHCHR, amesema licha ya shambulizi la jana lililokatili maisha ya zaidi ya watoto 21 waliokuwa kwenye basi mjini Saada,  makombora yanayoendelea kurushwa tangu wiki  iliyopita, yanazidi kusababisha sio mafaa  kwa raia na watoto, bali kuathiri pia miundombinu nchini humo. 

"Kuhusu mashambulizi ya wiki iliyopita katika bandari ya Hudaydah, ofisi yetu Yemen imerekodi  kuwa raia 41 , ikiwa ni pamoja na watoto sita na wanawake wanne, waliuawa na wengine 111 walijeruhiwa, kati yao 19 nin watoto na wanawake watatu," amesema Bi. Throssel.

Naye Christophe Boulierac  ambaye ni msemaji wa UNICEF amesema  wafanyakazi wa shirika hilowalioko Yemen wameripoti machafuko makubwa, ikiwa ni pamoja na  hali ya kutisha   katika hospitali ambapo waathirika wanaendelea kutibiwa, na kuongeza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka ...

 

Mgao wa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji huko Yemen. Mgao huu hupatikana kwenye kituo kinachosaidiwa na UNICEF huko Hudaidah.
UNICEF
Mgao wa misaada ya kibinadamu kwa wahitaji huko Yemen. Mgao huu hupatikana kwenye kituo kinachosaidiwa na UNICEF huko Hudaidah.

 Amesema "tunaamini  kwamba shambulizi hili ni baya zaidi tangu 2015. Kwa kuangalia shambulizi hili la basi, UNICEF tunaamini kuwa haijawahi kutokea idadi kama hiyo ya watoto kupoteza maisha katika tukio kama hili hapo awali"

Msemaji huyo wa UNICEF akaongeza kuwa , "kila siku nchini  Yemen, watoto wanakabiliwa na  njaa, watoto wanakufa kwa sababu ya vurugu na matokeo yake."

Kwa mujibu wa UNICEF, zaidi wa watoto milioni 1.8 wako   hatari kuambukizwa magonjwa yakuhara na wengine milioni  1.3 ugonjwa wa vichomi.

Halikadhalika UNICEF inasema zaidi ya watoto milioni nne wanahitaji msaada mkubwa wa elimu.