Sasa rasmi, Bi. Bachelet kuwa kamishna mkuu wa haki za binadamu wa UN

10 Agosti 2018

Mabibi na mabwana, nina furaha kubwa kutangaza kuwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeridhia uteuzi wangu wa Michelle Bachelet kuwa Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa  Umoja wa Mataifa!

Ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani, punde tu baada ya Baraza Kuu la umoja huo kumthibitisha Bi. Bachelet kutoka Chile kuwa mrithi wa Zeid Ra’ad Al Hussein anayeng’atuka mwezi huu.

Amemmiminia sifa kem kemi akisema kuwa, "Bi. Bachelet amekuwa ni mtu muhimu sana huko nchini kwake Chile vivyo hivyo kwa Umoja wa Mataifa. Nyumbani amepitia chungu na tamu, akiwa ni mwanamke wa kwanza kuwa rais wan chi hiyo, lakini pia manusura wa utakili wa mamlaka ambazo zilizomlenga yeye na familia yake miongo mingi iliyopita.”

 Na kama hiyo haitoshi, amesema Bi. Bachelet amepitia utawala wa kidikteta, na kama daktari anafahamu mapito ya watu wanaohaha kupata huduma za afya na kufurahia haki zao za kiuchumi na kijamii. Bwana Guterres amesema Kamishna Mkuu  huyo mteule wa haki za binadamu anachukua nafasi hiyo katika kipindi ambacho chuki imeshamiri huku haki za binadamu zikisiginwa akisema kuwa Bi. Bachelet anafahamu wajibu wa uongozi wa kitaifa na kimataifa.

“Ili kukabili mapito haya, tunahitaji mchechemuzi thabiti wa haki zote za binadamu- haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Tunahitaji mtu ambaye anaweza kuhakikisha uzingatiaji wa mifumo ya  haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa," amesema Katibu Mkuu.

 Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Bwana Zeid kwa uongozi, upendo na stadi zake akihudumu kama Kamishna wa haki za binadamu kwa kipindi chote cha miaka minne, akimtakia yeyé na familia yake kila la kheri.

Wakati huo huo, Bwana Zeid ametoa taarifa ya kupongeza uteuzi wa mrithi wake, Bi. Bachelet akisema ana sifa zote ikiwemo ujasiri, uvumilivu, upendo na azma ya dhati katika kutetea haki za binadamu popote pale ulimwenguni.

Bi. Bachelet alikuwa Rais wa Chile kwa awamu mbili ambapo ni kuanzia mwaka 2006 hadi 2010 na 2014 hai 2018 na anakuwa Kamishna wa 7 wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa tangu ofisi hiyo ianzishwe mwaka 1993.

Wengine ni Zeid Ra’ad Al Hussein Septemba 2014-2018, José Ayala-Lasso 1994-97,  Mary Robinson 1997-2002, Sergio Vieira de Mello 2002-03, Louise Arbour 2004-08, na Navi Pillay 2008-14.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter