Vijana waliookolewa pangoni Thailand wapatiwa uraia
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limekaribisha hii leo uamuzi wa serikali ya Thailand ya kuwapa uraia vijana watatu na kocha wao wa soka , ambao hivi karibuni waliokolewa kutoka pangoni huko Chiang Rai katika operesheni isiyo ya kawaida iliyoongozwa na jeshi la nchi hiyo.
Carol Batchelor ambaye ni Mshauri Maalum wa UNHCR juu ya masuala ya watu wasiokuwa na utaifa amesema, “kwa kuwapatia uraia wavulana hawa na kocha wao, Thailand imewapa fursa ya sio tu kukamilisha ndoto zao balipia kufikia malengo kadri ya uwezo wao hapo baadaye zaidi na kufikia uwezo.”
Ameongeza kuwa Thailand imewapa utambulisho rasmi ambao ni njia ya kufikia matarajio yao na kushiriki kikamilifu kama wanachama kamili katika jamii zao.
Aidha Bi Batchelor amesema kuwa watu ambao hawatambuliki rasmi na taifa lolote huchukuliwa kama “wasio na utaifa “ na mara nyingi hujikuta bila haki wala huduma za msingi.
Amesema watu hao hawawezi kusafiri, kuolewa, kumiliki mali au kuajiriwa katika jamii wanamoishi na kwamba mara nyingi matatizo yao huwa hayapatiwi ufumbuzi.
UNHCR inasema kuwa Thailand imekuwa mstari wa mbele kikanda katika kuchukua hatua ya kukomesha hali ya watu kukosa utaifa ambapo watu wapatao 100,000 wamepatiwa uraia wa nchi hiyo tangu mwaka 2008.
Halikadhalika serikali hiyo imejitolea kutafuta ufumbuzi wa kitaifa kwa watu 480,000 ambao hawana utaifa ifikapo mwaka 2024.
Ni kwa mantiki hiyo UNHCR na washirika kupitia kampeni ya “I belong” kwa Kiswahili “Mimi ni wa” itaendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ya Thailand katika kutokomeza hali ya kutokuwa na utaifa kwenye ukanda huo.