Kitendo cha Zambia kumrejesha kinguvu nyumbani mwanasiasa hakikubaliki-UNHCR

9 Agosti 2018

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kurejeshwa nyumbani kinguvu kwa raia mmoja wa Zimbabwe aliyekuwa anasaka hifadhi Zambia.

UNHCR kupitia taarifa yake ya leo imetoa wito kwa Zambia ifanye uchunguzi  wa haraka kuhusu  tukio hilo.

Inaripotiwa kuwa hapo jana mwanasiasa mmoja mwandamizi wa Zimbabwe, ambaye hakutajwa jina, alifika mpakani mwa Zimbabwe na Zambia na  kueleza nia yake ya kupewa hifadhi ya kisiasa nchini humo.

Hata hivyo maafisa wa Zambia hii leo wamemkabidhi kwa mamlaka za nchi  yake licha ya mahakama ya Zambia kuamua vinginevyo.

UNHCR inasema kumrejesha nyumbani bila hiari mkimbizi yeyote au msaka hifadhi ni ukiukwaji mkubwa wa  sheria ya kimataifa ya wakimbizi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud