Michelle Bachelet kuchukua usukani wa ofisi ya haki za binadamu:UN

Michelle Bachelet Rais wa Chile ndiye atakayevaa kofia ya Kamishina Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa baada ya kamishna wa sasa Zeid Ra’ad al Hussein kumaliza muda wake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amelijulisha Baraza Kuu kuhusu nia yake ya kumpendekeza Rais huyo wa zamani wa Chile kuchukua hatamu za ofisi ya haki za binadamu.
Kupitia taarifa ya msemaji wake, Katibu Mkuu amelijulisha Baraza Kuu baada ya majadiliano na wenyeviti wa makundi ya kikanda ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Bi. Bachelet amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo kuwa Rais wa Chile katika vipindi viwili totaiuti, kuanzia 2006 hadi 2010 na mwaka 2014 hadi 2018. Na mwaka 2010 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alimteua kuwa mkurugenzi mtendaji wa kwanza wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake (UN-Women).
Pia aliwahi kushika nafasi za uwaziri nchini Chile ikiwemo waziri wa ulinzi mwaka 2002-2004 na waziri wa afya mwaka 2000-2002.