Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka elimu chini ya miti hadi ya ndani ya darasa Yambio.

Watoto wakiwa ndani ya darasa wakisoma. Wenzao sehemu za Sudan Kusini husoma wakiwa chini ya miti.
Photo: UNICEF/Eldson Chagara
Watoto wakiwa ndani ya darasa wakisoma. Wenzao sehemu za Sudan Kusini husoma wakiwa chini ya miti.

Kutoka elimu chini ya miti hadi ya ndani ya darasa Yambio.

Utamaduni na Elimu

Zaidi ya watoto 500 wa mji wa Yambio katika jimbo la Gbudue nchini Sudan Kusini ambao awali walikuwa wanasomea chini ya miti sasa mwelekeo wao wa elimu umenyooka baada kufunguliwa kwa jengo jipya lenye vyumba vinne vya madarasa.

Jengo hilo la shule ya chekechea na ya msingi ya United, kwa kiingereza United Nursery and Primary Schoo, limejengwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS  kupitia mradi wa kuleta matokeo ya haraka, au Quick Impact.

Lucy Samuel ambaye ni  mmoja wa wanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo  amesema amejawa na furaha kwa sababu wamejengewa shule nzuri ya wao kujifunzia.

Taarifa ya UNMISS imesema shule hii ilianza mwaka jana ikiwa na wanafunzi 180 wakisomea chini ya miti ambapo hivi sasa imepiga hatua na idadi ya watoto wanaojiunga kutaka kusoma ikiongezeka hadi kufikia zaidi ya watoto 500.

 Yambio nchini Sudan Kusini. baadhi ya maeneo wanafuzxi walikuwa akisomea chini ya miti, lakini UNMISS inasadia kujenga madarasa
UN /Nektarios Markogiannis
Yambio nchini Sudan Kusini. baadhi ya maeneo wanafuzxi walikuwa akisomea chini ya miti, lakini UNMISS inasadia kujenga madarasa

 

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Seba Murangi, amesema kuwa wakati madarasa yaliyopokuwa chini ya miti idadi ya wanafunzi ilikuwa ndogo, lakini sasa wazazi wanapata mwamko wa watoto wao kupata elimu kutokana na maboresho yaliyofanyika.

Shule hii ni ya kwanza ya aina yake kwenye eneo la Ikpiro mjini Yambio na maafisa  wake  wanatarajia idadi ya wanafunzi kuongezeka na hivyo kutoa fursa zaidi ya watoto kusoma.

UNMISS imetekeleza miradi 16 ya matokeo ya haraka kwenye ukanda wa Equatoria Magharibi tangu mwaka 2012.

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa  shule, vituo vya polisi, vituo vya kupatia  maji safi ,madaraja na pia huduma za kujisafi.