Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzuia kuingia mafuta Gaza ni hatari inayoweka rehani maisha ya mamilioni ya wagonjwa:McGoldrick

Picha ya upande wa Palestina wa Karem Shalom ambako bidhaa zinaingia na kutoka kati ya Israel na Gaza , ambapo sehemu iliteketezwa kwa moto na Wapalestina, na kuathiri uwezo wake wa kusafirisha baadhi ya bidhaa cha chakula ikiwemo pia mafuta ya dharura. 1
Picha na UN
Picha ya upande wa Palestina wa Karem Shalom ambako bidhaa zinaingia na kutoka kati ya Israel na Gaza , ambapo sehemu iliteketezwa kwa moto na Wapalestina, na kuathiri uwezo wake wa kusafirisha baadhi ya bidhaa cha chakula ikiwemo pia mafuta ya dharura. 1

Kuzuia kuingia mafuta Gaza ni hatari inayoweka rehani maisha ya mamilioni ya wagonjwa:McGoldrick

Amani na Usalama

Vikwazo dhidi ya kuingiza mafuta ya dharura yanayohitajika haraka Gaza, ni kitendo cha hatari ambacho kina athiri kubwa kwa haki za watu wa Gaza na kuyaweka rehani maisha yao.

Kauli hiyo imetolewa leo na Jamie McGoldrick ambaye ni mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa  (OCHA) kwenye maeneo yanayokaliwa ya Palestina, akisisitiza kwamba mustakhbali wa watu milioni mbili, nusu yao wakiwa ni watoto uko hatarini na kwamba “haikubaliki kwa Wapalestina walioko Gaza kila wakati kunyimwa haki za vitu vya msingi katika maisha”.

Wadau wa masuala ya afya, maji na usafi wamesema takribani lita 60,000 za mafuta ya dharura zinatakiwa haraka katika vituo 46 Gaza ili kuhakikisha kuendelea kwa huduma za msingi katika hospitali, mitambo ya maji na usafi kwa siku nne zijazo.

Mafuta yaliyopo na ambayo yanasubiri kuingizwa na mamlaka ya Israel, yanahitajika ili kuendesha genereta katika huduma hizo kufuatia tatizo sugu la umeme Gaza.

Ili kuepuka kufurika kwa maji taka katika makazi ya raia, manispaa ya Gaza imeamua kuelekeza zaidi ya lita 10,000 za maji taka kila siku Kaskazini mwa mji huo kuliko na mkusanyiko wa maji ya mvua hali inayo waweka katika hatari kubwa wakazi wa  maeneo ya jirani endapo maji hayo machafu yatafurika.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hivi sasa katika vituo 40 kati ya 132 vinatoa huduma za maji na usafi kiwango cha mafuta walichonacho kinatosheleza kwa siku moja au mbili tu, huku hospitali na vituo vingine vya afya vikilazimika kupunguza huduma na hospitali 5 zina uwezekano wa kufungwa katika siku tatu zijazo endapo mafuta ya dharura hayatoruhusiwa kuingia.

Kana kwamba janga hilo halitoshi, fedha kwa ajili ya kufadhili mafuta ya dharura nazo zitakwisha katikati ya mwezi huu wa Agosti, na dola milioni 4.5 zinahitajika ili kuendelea kutoa japo huduma ndogo za msingi katika vituo vya afya hadi mwisho wa mwaka huu.