Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola DRC: Chanjo yaanza kutolewa, WHO yahaha kuhakikisha usalama wa watoa huduma

Jinsi chanjo ya ebola inavyopatiwa binadamu ili kumkinga na ugonjwa huo. Pichani ni wakati wa mlipuko huko Equateur ambapo Dkt. Alhassane Toure anampatia chanjo mhudumu wa afya katika kituo cha Mbandaka, nchini DRC
WHO/Lindsay Mackenzie
Jinsi chanjo ya ebola inavyopatiwa binadamu ili kumkinga na ugonjwa huo. Pichani ni wakati wa mlipuko huko Equateur ambapo Dkt. Alhassane Toure anampatia chanjo mhudumu wa afya katika kituo cha Mbandaka, nchini DRC

Ebola DRC: Chanjo yaanza kutolewa, WHO yahaha kuhakikisha usalama wa watoa huduma

Afya

Baada ya kubaini aina ya virusi vya Ebola huko jimbo la Kivu Kaskazini, na kupata ridhaa ya kutoa chanjo ya mzunguko, shirika la afya ulimwenguni, WHO linaanza kutoa chanjo hiyo leo jimboni humo.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC chanjo dhidi ya virusi vya Ebola inaanza kutolewa leo kwenye maeneo ya Beni na Mangina jimboni Kivu Kaskazini, limesema shirika la afya ulimwenguni WHO wakati huu likihaha kuhakikisha vikundi vilivyojihami havikwamishi operesheni hiyo.

Msemaji wa WHO, Geneva Uswisi Tariq Jasarevic amesema utoaji chanjo unaanza na wahudumu wa afya na kisha kufuatia na watu 900 waliobainika kuwa na ukaribu na wagonjwa 43 ambao hadi sasa wanashukiwa kuwa na Ebola na 36 waliofariki dunia.

Amesema kinachowatia moyo ni habari ya kwamba aina ya virusi viliyothibitishwa Kivu Kaskazini ni tofauti na vile vya jimbo la Equateur kwa hivyo..

(Sauti ya Tarik Jasarevic)

“Chanjo inaanza leo tulikuwa na dozi 3200 za chanjo zilizobakia kutoka chanjo huko Equateur na  ambazo zililetwa Kivu Kaskazini.”

Kuhusu changamoto ya usalama Bwana Jasarevic amesema angalau huko Beni na Mangina wameweza kufika lakini kuna changamoto kufikia maeneo ya ndani zaidi wakati huu ambapo kiwango cha hatari ya usalama huko Kivu Kaskazini kutokana na uwepo wa vikundi vilivyojihami ni cha nne, kiwango ambacho amesema ni cha juu.

(Sauti ya Tarik Jasarevic)

“Kwa hivyo hivi sasa tunashirikiana na idara ya usalama la Umoja wa Mataifa kuangalia ni hatua gani  tunapaswa kuchukua kwa ajili ya wahudumu wanaokwenda eneo hilo kwa sababu usalama wao bila shaka ni muhimu sana.”

Huu ni mlipuko wa 10 wa Ebola nchini DRC ambapo mlipuko wa mwisho ulikuwa katika jimbo la Equateur na ulitangazwa kutokomezwa wiki mbili zilizopita.