Raia wa Venezuela wanaoomba hifadhi Brazil waongezeka kila uchao-UNHCR

7 Agosti 2018

Raia wa Venezuela 117,000 wameomba hifadhi mwaka huu hadi kufikia sasa, ikiwa ni idadi kubwa  kuliko raia wote wa nchi hiyo walioomba hifadhi kwa mwaka mzima wa 2017 limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, baada ya uamuzi wa mahakama kuu ya Brazil kutengua uamuzi wa jaji wa jimbo kufunga mpaka wa Kaskazini unaopakana na Venezuela.

William Spindler msemaji wa UNHCR mjini Geneva akizungumzia uamuazi huo wa kufungua tena mpaka amesema

(SAUTI YA WILKLIAM SPINDLER)

“UNHCR inakaribisha uamuzi wa mahakama Kuu ya Brazili wa kutengua uamuzi wa jaji wa serikali kwenye jimbo la mpakani la Roraima, wa kusitisha kuwaruhusu Wavenezuela kuingia nchini humo na kufunga mpaka.”

Ameongeza kuwa mamia ya raia wa Venezuela wanavuka mpaka na kuingia Roraima nchini Brazil kila siku wakisaka usalama.

Njia hiyo ilizuiliwa kwa muda Jumatatu wakati mpaka ulipofungwa kufuatia maamuzi ya jaji wa Roraima. Saa chache baadae uamuzi huo ukatenguliwa na mahakama kuu ya Brazil.

Zaidi ya Wavenezuela 200 hawakuweza kukamilisha uandikishwaji wa masauala ya uhamiaji baada ya mpaka kufungwa kwa muda Jumatatu lakini hawakurudishwa kwa nguvu au kufukuzwa limesema shirika la UNHCR.

Leo hii Brazil ni maskani ya waomba hifadhi 32,700 kutoka Venezuela na wengine 25,000 wana vibali halali vya kukaa nchini Brazil kwa sababu ya kufanya kazi, au wanamiliki makazi.

UNHCR imeongeza kuwa kuna taarifa ya mvutano mkubwa baina ya wageni hao na weyeji wakazi wa Roraima, huku ikielezwa kuna upungufu mkubwa wa chakula na madawa hali iliyosababisha ongezeko la mfumuko wa bei, mvutano wa kisiasa na machafuko Venezuela.

 

“kumekuwa na mvutano kiasi baina ya wenyeji na raia wa Venezuela, tunaelewa kwamba kumekuwa na wimbi kubwa lililoingia Roraima na ndio maana tunaisaidia serikali kukabiliana na hali hii.”

Kufikia sasa UNHCR imesha wasaidia Wavenezuela zaidi ya 800 kwenda kwenye maeneo mengine ya Brazil ili kupunguza mzigo kwa watu wa Roirama ambao wanaendelea kushuhudia idadi kubwa ya watu wanaosaka malazi kutoka Venezuela.

Shirika hilo linasema idadi kubwa ya Wavenezuela wanaokimbilia Brazil na nchi jirani ya Colombia wanahitaji msaada wa haraka wa nyaraka, malazi, chakula na huduma za afya vitu ambavyo UNHCR inatarajia kuvitoa kwa kushirikiana na serikali ya Brazil na washirika wengine.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Waliofurushwa makwao 2017 pekee ni sawa na idadi ya watu wa Thailand -UNHCR

Watu milioni 68.5 walikuwa wamefurushwa kutoka makwao hadi mwishoni mwa mwaka 2017, imesema ripoti mpya ambayo imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR.