Zaidi ya watoto 100 wanaotumikishwa vitani Sudan Kusini waachiliwa huru

7 Agosti 2018

Watoto wengine 128 wameachiliwa hii leo kutoka makundi  yanayojihami huko Sudan Kusini na hivyo kufanya idadi ya watoto walioachiliwa mwaka huu pekee kuwa zaidi ya 900.

Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF huko Sudan Kusini, Mahimbo Mdoe amesema hii ni mara ya nne kwa mwaka huu ambapo wanafanya tukio hilo la kupokea watoto waliosalimishwa na makundi yenye silaha.

Idadi kubwa ya watoto walioachiliwa walikuwa wanashikiliwa na kikundi cha SSNLM ambacoho mwaka 2016 kilitia saini na serikali ya Sudan  Kusini makubaliano  ya amani ilhali wengine waliachiliwa kutoka kikundi cha SPLA upande wa upinzani.

Amesema watoto zaidi wanaotumikishwa vitani na makundi hayo wanatarajiwa kuachiliwa huru katika miezi ijayo.

 “Maendeleo ya mwaka huu ya kupokea watoto hawa yanatupatia sababu ya kuwa na matumaini kuwa siku moja watoto wote 19,000 ambao bado wanatumimiswha kwenye vikundi vilivyojihami au jeshini hapa Sudan Kusini, wataachiliwa huru na kurejea kwenye familia zao,” amesema Bwana Mdoe huko Yambio jimbo la Gbudue.

UNICEF/Ohanesian
Mvulana mwenye umri wa miaka miaka 15 ambaye zamani alikuwa ametumikishwa jeshini akielekea shuleni Sudan Kusini.

Amesema ni kwa kuzingatia matumaini hayo kuwa wataendelea na kazi hiyo ya kufanikisha lengo hilo ili kutokomeza matumizi na utumikishaji wa watoto vitani.

Katika hafla ya kupokea watoto hao, watoto hao walisalimisha silaha, wakavua magwanda ya kijeshi na hatimaye kuvaa nguo za kiraia.

UNICEF inasema kinachofuatia ni uchunguzi wa afya zao na watoto hao watapatiwa msaada wa ushauri wa kisaikolojia na nasaha kama moja  ya mipango ya kuwajumuisha tena kwenye jamii.

Halikadhalika baada ya kurejea nyumbani, familia zao zitapatiwa msaada wa kutosheleza miezi mitatu kutoka shirika la mpango wa chakula duniani, WFP sambamba na mafunzo stadi kwa lengo la kuinua kipato cha familia na uhakika wa chakula.

Bwana Mdoe ameshukuru wadau wote waliofanikisha kuachiwa kwa watoto hao 128 ambapo 90 kati yao ni wavulana na 38 ni wasichana.

“Mashauriano baina ya pande zenye mzozo yanahitaji nguvu na azma ya  kutosha kutoka pande zote na ninashukuru sana wadau wetu,” amesema Bwana Mdoe.

Amesema UNICEF Sudan Kusini inahitaji dola milioni 45 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kufanikisha kuachiliwa na kujumuishwa kwenye jamii kwa watoto hao 19,000 ambao bado  wanashikiliwa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud