Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Ebola Kivu Kaskazini kuanza wiki hii- WHO

Vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinapakuliwa huko Mavivi jimbo la  Kivu Kaskazini mnamo Agosti 2018.
MONUSCO-AVIATION
Vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinapakuliwa huko Mavivi jimbo la Kivu Kaskazini mnamo Agosti 2018.

Chanjo dhidi ya Ebola Kivu Kaskazini kuanza wiki hii- WHO

Afya

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC serikali na wadau wake wakiwemo Umoja wa Mataifa wanaendelea na harakati za kudhibiti kuenea zaidi kwa ugonjwa wa Ebola wakati huu ambapo idadi ya watu waliofariki dunia kwenye jimbo la Kivu Kaskazini ni 34.

Wadau hao ni pamoja na shirika la afya ulimwenguni, WHO ambapo msemaji wake huko Geneva, Uswisi Tariq Jasarevic amewaambia waandishi wa habari kuwa kati ya vifo hivyo 34 visa vilivyothibitishwa kuwa ni Ebola ni 16 pekee.

Amesema sasa wanaendelea na harakati za kusaka watu waliokuwa karibu na wagonjwa na waliofariki dunia sambamba na kueliemisha umma jinsi ya kuepukana na ugonjwa huo na zaidi  ya yote.

(Sauti ya Tariq Jasarevic)

“Maabara iliyoko kwenye gari imeshaanza kazi tangu tarehe pili mwezi Agosti. Kazi ya kubaini watu waliokuwa karibu na wagonjwa imeanza na zaidi ya watu 900 wamesajiliwa huko Mangina ambako ni kitovu cha mlipuko kilichopo kilometa 30 kutoka Beni. MSF wameanzisha kituo cha matibabu huko Mangina ilhali ALIMA wameweka kituo cha tiba huko Beni.”

Kuhusu chanjo, amesema inatarajiwa kuanza wiki hii na vifaa kama vile majokofu ya kuhifadhi na mabomba ya sindano tayari yamewasili.

(Sauti  ya Tariq  Jasarevic)

“Chanjo itaanza na wahudumu wa afya halafu watu waliokuwa na ukaribu na wagonjwa na sasa tuna dozi 3000 za chanjo Kinshasa na tunafahamu kuwa kampuni ya chanjo inazo  nyingine na italeta iwapo zitahitajika.”

Wakati hoja ya suala la usalama huko Kivu Kaskazini ilikuwa ni moja ya changamoto tajwa, WHO imesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO uko sambamba katika kufanikisha operesheni za kudhibiti Ebola.

Amezungumzia pia mazishi salama akisema yameanza huko Beni kwa wagonjwa waliofariki dunia akisema wameweka mfumo kuhakikisha kwamba yanafanyika kwa usalama na kiutu.

Halikadhalika amesema wamebaini maeneo 28 ambayo yanatumika kuingia na kutoka jimbo la Kivu Kaskazini ambapo wanafanya ufuatiliaji ikiwemo kupima joto la watu na kujaza fomu iwapo mtu anashukiwa ana Ebola anaelekezwa hospitali ya kwenda kupata tiba.

 “Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus na Naibu Mkurugenzi Mkuu anayehusika na masuala ya dharura, Dkt. Peter Salama watasafiri kuelekea DRC siku ya Alhamisi ili kujionea wenyewe harakati za kudhibiti Ebola,” amesema Bwana Jasarevic.

Tayari WHO  imetoa dola milioni 2 kutoka mfuko wake wa dharura ili kukabiliana na mlipuko huo wa 10 wa Ebola nchini DRC.