Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo yaendelea Yemen huku mitutu ya bunduki ikimiminwa

Mvulana akipewa chanjo dhidi ya kipindupindu mjini Aden nchini Yemen mnamo Mei 7, 2018 ambapo kwa sasa kampeni ya chanjo inaendelea.
UNICEF/Sadeq Al-Wesabi
Mvulana akipewa chanjo dhidi ya kipindupindu mjini Aden nchini Yemen mnamo Mei 7, 2018 ambapo kwa sasa kampeni ya chanjo inaendelea.

Chanjo yaendelea Yemen huku mitutu ya bunduki ikimiminwa

Afya

Licha ya makombora kuendelea kuporomoshwa huko Hudaidah kusini magharibi mwa Yemen kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kihouthi, mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la afya WHO, la kuhudumia watoto UNICEF na la kuhudumia wakimbizi UNHCR, yanaendelea na kampeni ya chanjo dhidi ya mlipuko wa kipindupindu.

Akihojiwa kwa njia ya simu na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa kutoka Yemen, kuhusu utoaji wa chanjo hiyo wakati huu ambapo zaidi ya watu laki mbili wameshapatiwa chanjo tangu kampeni hii ianze tarehe 4 mwezi huu, Adnan Abdelfattah ambaye ni msemaji wa UNICEF  Yemen amesema…

 (Sauti ya Adnan Abdelfattah)

“Kampeni inafanyika huku milio ya risasi na makombora ikiendelea kusikika. Wafanyakazi wa afya wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wimbi la wakimbizi wa ndani. Kama unavyojua, mkoa wa AlHuddah sasa unakabiliwa na mapigano makali kati ya pande kinzani  yavikundi mbalimbali."

Kampeni ya kwanza ya chanjo dhidi ya kipindupindu ilifanyika mwezi mei mwaka huu, chini ya usimamizi wa WHO, UNICEF katika kitongoji cha Aden ambacho kilikabiliwa na hatari kubwa ya maambukizi.

Yemen imeendelea kukabiliwa na milipuko ya kipindupindu miaka ya hivi karibuni ambapo zaidi ya watu milioni 1 wanasadikiwa kuambukizwa na 2316 wamepoteza maisha tangu mwezi aprili mwaka 2017.