Wasomali zaidi ya 2000 warejea nyumbani toka Yemen kwa msaada wa UNHCR

7 Agosti 2018

Wakimbizi wa Kisomali 116 wamerejea nyumbani wiki hii kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na kufanya idadi ya wakimbizi waliorejea nyumbani toka Yemen tangu 2017 kufikia zaidi ya 2000.

Kwa mujibu wa shirika hilo wakimbizi hao waliwasili kwenye bandari ya Berbera Somalia baada ya kuondoka Aden nchini Yemen siku ya Jumapili.

UNHCR inasema mpango wa kuwarejesha wakimbizi hao kwa hiyari ulioanza mwaka jana unafanywa kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na serikali ya Yemen. William Spindler msemaji wa UNHCR mjini Geneva Uswisi amesema, "Mwaka huu hadi kufikia sasa Wasomali 1321 wakiwemo 116 walioondoka Jumapili wamerejea mwakwao nchini Somalia. Kwa miezi miwli iliyopita hali ya hewa ilizuia boti kusafiri, miongoni mwa wakimbizi hao ni wanawake ambao ni walezi wa familia wanaotarajiwa kwenda kujiunga na ndugu zao, wanafunzi wanaotarajia kurejea masomoni na mgonjwa mahtuti aliyesafiri na mwanae, wanafamialia na madaktari.”

Yemen hivi sasa inahifadhi zaidi ya wakimbizi 270,000, huku 256, 363 kati yao wakiwa ni Wasomali. Alimia 45 ya wakimbizi hao wanahifadhiwa katika kambi ya Kharaz Kusini mwa nchi hiyo na wengine katika makazi ya Basateen mjini Aden.

Baada ya kuwasili nyumbani Somalia wakimbizi hao wanapatiwa msaada wa fedha, pia vifaa vya nyumbani, chakula kutoka kwa shirika la mpango wa chakula duniani WFP, na fedha kwa ajili ya shule kwa watoto wa shule za msingi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud