Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tetemeko Indonesia, UN iko tayari kutoa msaada

Wafanyakazi wa msalaba mwekundu nchini Indonesia wakisaidia kuondoa watoto kutoka kisiwa cha Lambok kufuatia tetemeko la ardhi la Agosti 5, 2018.
Indonesian Red Cross
Wafanyakazi wa msalaba mwekundu nchini Indonesia wakisaidia kuondoa watoto kutoka kisiwa cha Lambok kufuatia tetemeko la ardhi la Agosti 5, 2018.

Tetemeko Indonesia, UN iko tayari kutoa msaada

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umesema uko tayari kutoa msaada wa uokoaji na ile ya kibinadamu kufuatia tetemeko la ardhi lililokumba Indonesia siku ya jumapili. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo kwenye taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wake hii leo kutokana na vifo na majeruhi waliotokana na tetemeko hilo lililokuwa na ukumbwa wa 7.0 katika kipimo cha richa. Pamoja na kusema ya kwamba wako tayari kutoa msaada iwapo wataombwa kufanya hivyo, ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na serikali ya Indonesia huku akitakia majeruhi ahueni ya haraka.

Yaelezwa kuwa zaidi ya watu 90 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa baada ya tetemeko hilo kukumba eneo la Lombok.

Tetemeko hilo lilizusha taharuki kubwa huku maelfu ya watu wakikimbia nyumba zao na kulala barabarani usiku kucha kuhofia maisha yao, na mamia ya majeruhi walilazimika kupatiwa matibabu katika maeneo ya wazi kwa kuhofia kujeruhiwa zaidi

Watu wa kujitolea na wafanyakazi wa chama cha msalaba mwekundu nchini Indonesia ndio wamekuwa wakisaidia waathirika na kuwahamisha manusura kutoka maeneo ya pwani baada ya serikali kutoa tahadhari ya tsunami ambayo baadae ilifutwa.

Majeruhi wa tetemeko la arshi la Agosti 5, 2018 Lombok Kaskazini anahamishwa na wafanyakazi wa msalaba mwekundu.
Indonesian Red Cross
Majeruhi wa tetemeko la arshi la Agosti 5, 2018 Lombok Kaskazini anahamishwa na wafanyakazi wa msalaba mwekundu.

 

Chama hicho kinasema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kufuatilia tetemeko hilo ambalo lilitikisa pia katika majimbo ya jirani ya Bali na Surabaya.

Hadi sasa chama cha msalama mwekundu nchini humo kimeshagawa mablanketi kwa waathirika ambao wanalala nje na inatoa msaada wa kisaikolojia. Kikubwa kwa sasa ni kuendelea kusaka manusura, na kukidhi mahitaji ya msingi kama chakula, huduma za afya , maji, mablanketi , magodopro na mahema.

Zaidi ya watu 100 wa kujitolea kutoka chama cha msalaba mwekundu wako katika eneo la tukio na wengine 140 wanatarajiwa, pia mashirika mengine ya misaada likiwemo la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la mpango wa chakula WFP na mashirika mengine ya kibinadamu yanatarajiwa kujumuika katika kutoa msaada kwa waathirika.

Hili ni tetemeko la pili ndani ya mwezi mmoja lingine lilizuka Julai 29.