Brazil kwanza timizeni haki za binadamu, kubana matumizi kutafuata-UN

3 Agosti 2018

Kundi la wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Brazil kutafakari upya mipango yake ya kubana matumizi na kutoa kipaumbele  kwanza kwa haki za binadamu za watu wake ambao wanaathirika na mipango hiyo ya sera za kiuchumi.

Takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya vifo vya watoto inaongezeka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 26. Ongezeko hilo lililochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mlipuko wa homa ya Zika na mgogoro wa kiuchumi linatia wasiwasi mkubwa wamesema wataalamu hao,  hususan kwa mifumo ya afya ya jamii, na será zingine za  masuala ya jamii ambayo yanaathiri kwa kiasi kikubwa wajibu wa serikali katika kutekeleza na kuhakikisha haki za binadamu kwa wote na hasa wanawake na watoto.

Wataalamu hao wameongeza kuwa “baadhi ya maamuzi na mipango ya kubana matumizi iliyopitishwa miaka iliyopita inakiuka haki nyingi za msingi ikiwemo haki za nyumba, chakula, maji , usafi, elimu, hifadhi ya jamii na afya, na inaongeza adha katika hali ambazo tayari zilikuwa mbaya.”

Wakitoa mfano wamesema “Wanawake na watoto wanaoishi katika umasikini ni miongoni mwa wanaoathirika zaidi na mipango hiyo, kwani wengi ni Wabrazil wenye asili ya Afrika , watu wa vijijini na watu wanaoishi katika mitaa ya mabanda au makazi yasiyo rasmi.”

Pia wamesema wanasikitishwa kwamba,  juhudi za kuwa na sera zitakazoshughulikia ubaguzi dhidi ya wanawake na makundi mengine yasiyojiweza sio endelevu.

Wataalamu hao ni pamoja na anayeshughulikia madeni ya nje na haki za binadamu, wa haki za maji salama ya kunywa na usafi, kundi la wanaoshughulika na masuala ya ubaguzi dhidi ya wanawake katika sheria, wa haki ya chakula , wa haki ya nyumba bora, wa haki ya afya ya mwili na akili na wa haki ya elimu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud