Tutafanya kila tuwezalo kulinda watu dhidi ya Ebola Kivu Kaskazini- WHO

3 Agosti 2018

Shirika la afya Ulimwenguni WHO, limesema litafanya kila liwezalo kudhibiti kuenea kwa mlipuko wa Ebola ambao umethibitishwa huko jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Dkt. Peter Salama ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa WHO anayehusika na masuala ya dharura amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa tayari wameanza kuweka  mikakati madhubuti ya kudhibiti mlipuko huo wa 10 nchini DRC wakati huu ambapo kuna ripoti za vifo ambavyo havijathibitishiwa kuwa vimetokana na Ebola.

(Sauti  ya Dkt. Peter Salama)

 

Dr Peter Salama, naibu Mkurugenzi  Mkuu wa WHO masuala ya dharura WHO
UN News/Daniel Johnson
Dr Peter Salama, naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO masuala ya dharura WHO

 “Tunafahamu kwa mfano kwamba kuna vifo vya watu 20 ambavyo tupo katika harakati za kuthibitisha kama wote wamefaridi dunia kutokana na Ebola au la. Hata hivyo tunatarajia idadi hiyo kuongezeka katika siku au wiki zijazo.

Dkt. Salama pia amegusia changamoto ya usalama ambayo wanakabiliana nayo huko Kivu Kaskazini akisema ni kizingiti kikubwa katika kufikia jamii pamoja na ikizingatiwa pia kuna askari 20,000 wa Umoja wa Mataifa wanaolinda amani jimboni humo.

 (Sauti ya Dkt. Peter Salama)

 “Tumefanya tathmini  ya tishio la maambukizi na kubaini kuwa hatari ni kubwa na ni ya juu sana kwa ngazi za kitaifa, na pia kwa ngazi ya kikanda, na ni ya chini kwa ngazi ya kimataifa.”

Wakati huo huo ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani  nchini DRC, MONUSCO umeshajipanga ili kuwezesha watoa huduma kukabiliana na changamoto ya usalama wakati wa harakati dhidi ya Ebola.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter