Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili huu Yemen unasikitisha na ni lazima ukomeshwe-UN

Hospitali ya Al Thawra, Hodeidah nchini Yemen. 115 Aprili 2017
OCHA/Giles Clarke
Hospitali ya Al Thawra, Hodeidah nchini Yemen. 115 Aprili 2017

Ukatili huu Yemen unasikitisha na ni lazima ukomeshwe-UN

Amani na Usalama

Hospital kubwa kabisa nchini Yemen ya Al Thawra iliyoko mjini Hodeidah imeshambuliwa usiku wa kuamkia leo na kusababisha vifo na majeruhi, kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA.

Mashambulizi hayo ya anga yamesambaratisha pia miundombinu na majengo mengine katika maeneo ya karibu na hospital hiyo. Mratibu wa masuala ya kibinadamu Yemen Lise Grand amesema hali hiyo ni ya “kushangaza na kusikitisha , hospital zinalindwa chini ya sheria za kimataifa za binadamu na hakuna chochote kinachohalalisha upotevu huo wa maisha ya binadamu.” Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis hii leo kuhusu shambulio hilo msemaji wa OCHA Jens Laerke amenukuu tarifa ya Lise Granda na kusema

(SAUTI YA JENS LEARKE)

Al Thawra ndio hospital kubwa nchini Yemen na moja ya hospital chache zinazofanya kazi katika eneo hilo. Ina moja ya vituo bora zaidi vya kutibu kipindupindu mjini humo, mamia kwa maelfu ya watu wanategemea hospitali hiyo ili kuishi. Kila siku wiki hii tumeshuhudia visa vipya Hodeidah, na sasa hili. Athari za shambulio hili zinatisha na kila juhudi tunazojaribu kufanya kwa ajili ya mlipuko huu mbaya zaidi wa kipindupindu duniani ziko hatarini.”

Ameongeza kuwa pande zote kinzani katika mzozo wa Yemen zina wajibu kimataifa kuwalinda raia na miundombinu yao kwa kufanya kila liwezekanalo , na huo sio wajibu wa hiyari bali ni wa lazima.

Hivi sasa mgogoro wa Yemen ndio mbaya kuliko yote duniani , watu milioni 22 sawa na asilimia 75 ya watu wote wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Na Wayemen zaidi ya 28,000 ama wameuawa au kujeruhiwa tangu kuzuka kwa mgogoro 2015.