Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini yaweka vikwazo vya kuuza mkaa nje ya nchi

Mkaa, nishati ambayo inatumiwa na wengi lakini madhara yake kwa mazingira ni makubwa. (Picha:UN /Stuart Price)

Sudan Kusini yaweka vikwazo vya kuuza mkaa nje ya nchi

Tabianchi na mazingira

Serikali ya Sudan Kusini imetangaza udhibiti wa uuzaji wa mkaa nje ya nchi hiyo kuanzia mwezi uliopita wa Julai. Hatua hiyo iliyotangazwa na Waziri wa Biashara wa Sudan Kusini Dkt. Moses Hassan Tiel imetaka maafisa wote wa biashara nchini humo walioko katika vituo vya mipakani pamoja na vyombo vya usalama, vya kuzuia biashara ya magendo na mashushu wa masuala ya kiuchumi kuhakikisha udhibiti huo unatekelezwa nchini kote.

 

Taarifa ya shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP linasema lengo la hatua hiyo ni kubadili mwelekeo au kupunguza uharibifu wa mazingira hususan ukataji miti ulioshamiri nchini humo, ambapo agizo la sasa ni la pili baada ya lile la mwaka 2015 lililopiga marufuku ukataji haramu wa magogo na uuzaji nje ya nchi magogo pamoja na mkaa.

Kwa  mujibu wa utafiti wa  pamoja wa mwaka 2015 wa UNEP na serikali ya Sudan Kusini aslimilia 88 ya kaya , na pia asilimia sabini na tano ya biashara katika mji mkuu Juba hutegemea nishati ya mkaa, huku  asilimia 15 tu ya kaya  ikitumia kuni.

Kama hiyo haitoshi, ripoti ya taifa kuhusu hali ya mazingira iliyozinduliwa mwezi Juni mwaka huu wa 2018 inaonyesha kuwa matumizi ya kuni  na mkaa nchini humo  hutokana na zaidi ya asilimia 80 ya miti yote iliyotumiwa sudan Kusini, na kiwango cha ukataji miti kila mwaka ni kati ya asilimia 1.5 na 2.

Rais wa Sudan Kusini, Bwana Salva Kiir Mayardit katika utangulizi wa ripoti hiyo amesema “Mpaka kufikia mafanikio, kuna shinikizo kubwa kwenyemaliasili hususani kwenye misitu, kwa kuwa asilimia 99 ya wananchi wa Sudan Kusini hutegemea misitu kwa ajili ya nishati na  mbao za ujenzi na samani,”

 

Image
Ukataji miti kwa ajili ya mkaa.(Picha:World Bank/video capture)

UNEP inasema licha ya kuwa na kiwango cha chini kabisa cha idadi ya watu barani Afrka, ambacho ni cha watu chini ya 13 kwa kilomita ya mraba, misitu ya Sudan Kusini bado inakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na matumizi ya kupindukia ya mkaa na kuni kama nishati mbadala.

Hata hivyo UNEP inasema tishio siyo matumizi ya mkaa ndani ya nchi pekee, bali pia ongezeko la mahitaji ya mkaa nchi jirani za Uganda, Sudan na Mashariki ya Kati.

Naye  Arshad Khan ambaye ni meneja wa UNEP, Sudan  kusini amesema, "Tunaendelea kufanya kazi na serikali ya Sudan Kusini, sekta binafsi, na mashirika ya kiraia, ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya nchi  katika siku zijazo kwa kuendeleza usimamizi bora wa mazingira

UNEP imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini Sudan Kusini tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011 ikiendeleza ufahamu wa mazingira kwa kiwango cha kitaifa na kusaidia serikali na watu wa Sudan Kusini.