Ebola yaibuka Kivu Kaskazini, UN yachukua hatua

2 Agosti 2018

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, umewasili jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ili kusaka mbinu za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Hatua hii inafuatia tangazo la jana la serikali ya DRC ya kuthibitisha visa vinne kati ya sita vya Ebola kwenye miji ya Beni na Goma jimboni humo, ikiwa ni siku chache tu baada ya Ebola kutangazwa kutokomezwa rasmi kwenye jimbo la Equateur nchini humo.

Timu iliyowasili Beni, kilometa 30 kutoka eneo ambako visa vya Ebola vimeripotiwa ni kutoka Wizara ya afya ya DRC, WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Benki ya Dunia na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA.

Akihojiwa na Idhaa hii, msemaji wa WHO, Tarik Jasarevic amesema kinachofanyika sasa ni, "uchunguzi wa kitabibu ili kujaribu kubaini ni watu wangapi wanaweza kuwa wameambukizwa, watu waliokutana nao na kushirikiana na wahudumu wa afya katika mbinu za kudhibiti maambukizi na pia kushirikisha jamii.”

Hata hivyo amesema kuna changamoto ya kwamba, "Kivu Kaskazini ni eneo ambalo lisilo na utulivu na kuna mapigano tunatumai kuwa tutaweza kufika ipasavyo na kuweza kufanya vyema kama tulivyofanya jimbo la Equateur ambako miezi kadhaa iliyopita tuliweza kudhibiti mlipuko ambao ulitangazwa kutokomezwa wiki iliyopita.”

Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC
UNICEF/Mark Naftalin
Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC

Mapema akizungumzia taarifa hizo za kubainika tena kwa Ebola, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus, amesema kile kinachowatia moyo ni jinsi ambavyo serikali ya DRC imekuwa wazi katika kuchukua hatua na hata kuripoti kilichotokea.

Amesema ushirikiano wa karibu kati yao na serikali utasaidia kupambana na mlipuko wa sasa kama ilivyokuwa huko Equateur.

Naye Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema kwa kuwa ni hivi majuzi tu wamehitimisha harakati dhidi ya Ebola, watendaji pamoja na vifaa bado vipo na hivyo itawawezesha kuchukua hatua haraka.

Naye Dkt. Peter Salama ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema changamoto kubwa kukabili mlipuko huo itakuwa ni kufikia wagonjwa kwa sababu eneo hilo ni la mzozo.

Jimbo la Kivu Kaskazini lina wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni moja na linapakana na Uganda na Rwanda.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter