UN iko bega kwa bega na Afghanistan katika michakato ya chaguzi

1 Agosti 2018

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, umekaribisha hatua ya tume huru ya uchaguzi  nchini humo, IEC ya kutangaza kuwa uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 20 Aprili mwaka ujao wa 2019.

Tadamichi Yamamoto ambaye ni mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu nchini Afghanistan na pia mkuu wa UNAMA amesema tangazo la leo ni hatua muhimu ya kidemokrasia nchini Afghanistan na kwa mantiki hiyo, 

tunahimiza pande zote kinzani kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha kuwa muda na  masharti vinazingatiwa kwa ajili ya kufikia mafanikio katika uchaguzi ujao

Kwa mujibu wa takwimu ya IEC, zaidi ya wananchi milioni 8.9 wakiwemo wanawake milioni 3 wamejiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa wabunge na mabaraza la wilaya mwaka huu na pia kwa uchaguzi wa rais mwakani.

UNAMA inatarajia kufanyika kwa mchakato wa kina wa kuthbitisha wapiga kura ili kasoro zozote ziweze kushughulikiwa.

Bwana Yamamoto amesema kuwa UNAMA itakuwa na dhima isiyoegemea upande wowote katika kusaidia vyombo vya kusimamia uchaguzi  nchini Afghanistan pamoja na kuimarisha maadili, na mchakato wa uchaguzi ulio endelevu na jumuishi.

Amesisitiza kuwa ofisi yake imeazimia kushirikiana na taasisi za Afghanistan katika kutekeleza marekebisho yanayoimarisha uwazi na kujenga Imani ya wananchi kwenye mchakato wa demokrasia ikiwemo kuendeleza ushiriki wa wanawake kama wapiga kura na wagombea.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud