Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 13 wauawa Afghanistan, UN yalaani

Mitaa ya Jalalabad Afghanistan
UN Photo/Fardin Waezi)
Mitaa ya Jalalabad Afghanistan

Watu 13 wauawa Afghanistan, UN yalaani

Amani na Usalama

Watu 13 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa kufuatia shambulio la kujilipua lililofanyika leo huko Jalalabad nchini Afghanistan.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMA umelaani vikali shambulio hilo lililofanywa na wanaume wakiwemo washambuliaji wa kujilipua kwenye idara ya wakimbizi ya jimbo hilo la Jalalabad.

Shambulio la leo ambalo limedumu kwa saa kadhaa, ni miongoni mwa msururu wa mashambulizi yanayolenga raia na miundombinu ya kiraia.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Afghanistan ambaye pia ni mkuu wa UNAMa Tadamichi Yamamoto amesema jimbo hilo la Jalalabad na maeneo  ya jirani  limeshuhudia mashambulizi mengi hivi karibuni yakilenga raia na miundombinu ya kijamii ikiwemo shule, na hospitali.

Mapema wiki hii kituo cha mafunzo ya wakunga kilishabmuliwa ambapo Bwana Yamamoto amesema mashambulio hayo yanachukiza.

Ametaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria huku akisisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unataka pande zote kinzani huko Afghanistan kuzingatia wajibu wao wa kulinda raia.

Pamoja na kulaani ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa huku akitakia ahueni  ya haraka majeruhi.