Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi ya viwanda yatishia uwepo wa watu na wanyama Bangladesh

Simba marara hawa ni miongoni mwa wanyama ambao wako hatarini kutoweka iwapo Bangladesh itaendelea na miradi yake ya viwanda kwenye msitu huo wa Sundarbans
UN /John Isaac
Simba marara hawa ni miongoni mwa wanyama ambao wako hatarini kutoweka iwapo Bangladesh itaendelea na miradi yake ya viwanda kwenye msitu huo wa Sundarbans

Miradi ya viwanda yatishia uwepo wa watu na wanyama Bangladesh

Masuala ya UM

Bangladesh isitishe mara moja miradi yake ya viwanda kwenye msitu wa akiba wa Sundarbans ambao msitu mkubwa zaidi duniani wenye mikoko, amesema mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu na mazingira, John H. Knox.

Katika taarifa yake ya mwisho kwa umma iliyotolewa leo Geneva, Uswisi anapohitimisha jukumu lake la utaalamu maalum, Bwana Knox amesema kasi ya miradi ya viwanda kwenye msitu huo inatishia siyo tu bayonuai ya mimea na wanyama bali pia haki za binadamu za watu milioni 6.5.

Amesema maisha, makazi, afya, chakula na utamaduni wa watu hao vinategemea msitu huo wa akiba ambao umetanuka hadi ghuba ya Bengal, unatambuliwa kama moja ya maajabu ya kiasili ya dunia.

Msitu huo umetambuliwa hivyo kupitia mkataba wa kimataifa wa Ramsar juu ya uhifadhi wa maeneo oevu na pia shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamadunia, UNESCO limeutaja kuwa ni eneo la urithi wa dunia.

Halikadhalika msitu huo wa Sundarbans ni makazi ya wanyama walio hatarini kutoweka kama vile simba marara wa Bengali na pomboo wa mto Ganges.

Watafiti wakisafiri katika  msitu wa akiba wa Sundarbans nchini Bangladesh.
FAO/Mondal Falgoonee Kumar
Watafiti wakisafiri katika msitu wa akiba wa Sundarbans nchini Bangladesh.

 

Yaelezwa kuwa licha ya kamati ya UNESCO ya maeneo ya urithi wa dunia kupinga hatua hiyo, Bangladesh imeridhia zaidi ya miradi 320 ya ujenzi wa viwanda kwenye eneo hilo.

Miongoni mwa miradi hiyo ni mtambo wa kiwanda cha makaa ya mawe, mradi ambao umepitishwa bila kushirikisha umma na kuzingatia tathmini za athari za kimazingira.

“Tishio ambalo linatokana na uendelezaji wa viwanda kwenye msitu wa Sundarbans ni dhihirisho la vitisho ambavyo mazingira yanakumbana nayo ulimwenguni kote,” amesema Bwana Knox akiongeza kuwa bila shaka wananchi wa Bangladesh wanapenda ustawi wa kiuchumi lakini “ustawi wa muda mfupi bila kujali athari za mazingira ni sawa na kufukuza dhahabu ya mpumbavu,” amesema mtaalamu huyo.

Bwana Knox amesema ili kuwa na maendeleo endelevu ya dhati ni muhimu kulinda mazingira na kuhakikisha shaka na shuku zote zinazingatiwa na hivyo serikali ni lazima zisikilize sauti za wale ambao wanaathiriwa an miradi ya viwanda.

 “Mara nyingi, watu ambao wanapaza sauti zao kuhusu miradi ya maendeleo wanapuuzwa au hata kuonekana kuwa ni maadui wa serikali. Lakini kiukweli wanapaswa kuchukuliwa kama mabingwa wa maendeleo endelevu,” amesema mtaalamu huyo huru