Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urafiki na mshikamano vyaweza kuinusuru dunia:UN

Urafiki umetajwa kama sehemu muhimu ya kutatua migogoro duniani
© UNHCR/Sufyan Said
Urafiki umetajwa kama sehemu muhimu ya kutatua migogoro duniani

Urafiki na mshikamano vyaweza kuinusuru dunia:UN

Amani na Usalama

Dunia hivi sasa inakabiliwa na changamoto nyingi, migogoro na shinishizo ambazo zinasababisha mgawanyiko katika jamii umesema leo Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya urafiki.

Umezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na umasikini , machafuko, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambavyo vinakuwa kikwazo katika kutimiza malengo ya amani , usalama, maendeleo na utangamano miongoni mwa jamii duniani.

Na ili kuzikabili changamoto zote hizo, Umoja wa Mataifa unasema , ni lazima mizizi yake ikatwe kwa kuchagiza na kutetea ari ya mshikamano wa kibinadamu ambao uko katika mifumo mbalimbali ukiwemo wa kawaida kabisa ambao ni urafiki.

Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba kupitia urafiki kwa kujenga umoja, mshikamano na kuaminiana “tunaweza kuchangia mabadiliko ambayo yanahitajika haraka ili kufikia utulivu wa kudumu, kuwa na amani ambayo itatulinda sote na kuongeza ari kwa ajili ya kujenga dunia bora ambayo watu wote wanaungana kwa ajili ya mustakhbali bora kwa wote.”

Hivyo katika siku hii ya kimataifa ya urafiki , Umoja wa Mataifa unamhimiza kila mtu kutafakari mazuri yanayoletwa na urafiki badala ya matokeo ya kutokuwa nao katika Dunia ya sasa.