Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu ni lazima zizingatiwe:UN

Wasaka hifadhi  wakivuka mpaka wa Rio Grande kati ya Mexico na McAllen, katika jimbo la Texas.
Picha UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Wasaka hifadhi wakivuka mpaka wa Rio Grande kati ya Mexico na McAllen, katika jimbo la Texas.

Haki za waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu ni lazima zizingatiwe:UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Haki za waathirika wa biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu hususan wanawake na watoto zinapaswa kuzingatia , na nchi ni lazima zinafanye kila njia kuzuia na kupambana na janga hili la kimataifa.

Wito huo umetolewa na wataalamu wa haki za binadamu katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu ambayo kila mwaka huwa Julai 30.

Katika ujumbe wake kuhusu siku hii ,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema biashara hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaoathiri usawa, utulivu na kuchochea migogoro, na kuwafaidisha wachahe ambao hukandamiza na kuwapokonya haki za msingi waathirika ambao wengi ni wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM katika miaka 10 iliyopita takriban asilimia 80 ya safari za waathirika kimataifa zimepitia katika mipaka halali ikiwemo viwanya vya Ndege, bandarini na vituo halali vya ukaguzi mipakani.

Na robo tatu ya waathirika hao hunyanyaswa na kutumiwa bila kujua ikitolea mfano kisa cha msichana Khadija  aliyekuwa na umri wa miaka 14 ambaye alisafirishwa kiharamu na baba yake bila kujua  na kupitia mpaka baina ya Uganda na Kenya mwaka 2015, ili akaolewe nchini Kenya, na kwa bahati baada ya kugundua Khadija aliweza kuuarifu Ubalozi wakwe ambao ulimsaidia kupitia msaada wa IOM.

Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba wahusika wa biashara hii haramu ni lazima wavikishwe kwenye vyombo vya sheria na waathirika wahakikishiwe msaada ikiwemo wa kisaikolojia.

Naye Bi Maria Grazia Giammarinaro, mwakilishi maalumu wa ofisi ya  haki za binadamu kuhusu kupinga biashara za usafirisaji haramu wa binadamu amesema, miongoni mwa waathirika wa biashara hiyo ni wahamiaji, wakimbizi na wasaska hifadhi ambao wameacha nchi yao ya asili kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na migogoro ya kivita, maafa, mateso au umaskini uliokithiri, na nikama wameruka majivu na kukanyaga moto kwani "Wameacha nyuma kila kitu kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama wa  kijamii, na sasa wanakuwa waathirika tena  katika biashara haramu na unyanyasaji,"

Kaulimbiu mwaka huu katika "Siku ya kimataifa ya kupinga biashara  haramu ya Usafirishaji wa binadamu, ni kwamba, “hata wakati wa shida ujumuishwaji bila utengano ndio jibu.”