Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dr. Agnes Kijazi wa Tanzania kuwa mjumbe wa SDGs Umoja wa Mataifa

Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs  yako 17 .
UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yako 17 .

Dr. Agnes Kijazi wa Tanzania kuwa mjumbe wa SDGs Umoja wa Mataifa

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemteua Dr. Agnes Lawrence Kijazi ambaye ni mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa Tanzania,  kuwa mjumbe wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya wajumbe 10 itakayotoa msaada na ushauri wa masuala ya teknolojia (TFM) kwa Umoja huo.

Uteuzi huo umefanyika kufuatia uamuzi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhitaji kuwa na wajumbe kumi watakaoushauri umoja huo katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika  mchakato wa kufikia malengo ya maendeleo endelevu yaani SDGs.

Wajumbe hao 10 wameteuliwa kutoka asasi za kiraia, sekta binafsi na jumuiya ya masuala ya kisayansi. Mchakato wa uteuzi huo ulizingatia sifa mbalimbali ukiwemo ubobezi wa taaluma na heshima katika nchi zao ili waweze kutumikia kamati hii kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2018.

Dr. Kijazi hivi sasa ni kurugenzi mkuu wa mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)  na kupitia nafasi hiyo amekuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani (WMO). Pia ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na wa pili kwa Afrika nzima kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza kuu la WMO sambamba na kushika nyadhifa zingine za juu kwenye kamati za shirika hilo kikanda na kimataifa.

Dr. Kijazi mwenye stashahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya hali ya hewa ya kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town, nchini Afrika Kusini na akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya uongozi wa juu katika Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) Tanzania, ameweza kusaidia TMA kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuiwezesha nchi kupata cheti cha kimataifa katika utoaji huduma za hali ya hewa kwenye sekta ya usafiri wa anga mwaka 2008 na 2015.

TFM ni kamati iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015 kama chombo muhimu cha ushirikiano wa sekta za maendeleo duniani kwa lengo la kufikia malengo 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ifikapo 2030.