Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Syria waliokataliwa kuondoka eneo la mapigano wanatutia hofu: OCHA

Familia kutoka Quneira mashambani wakihaha wakitafuta mahala pa kukaa.Takriban watu 140,00 hawana makazi kusini magharibi mwa Syria na wanahitaji eneo salama la kupitia.
UNICEF/Alaa Al-Faqir
Familia kutoka Quneira mashambani wakihaha wakitafuta mahala pa kukaa.Takriban watu 140,00 hawana makazi kusini magharibi mwa Syria na wanahitaji eneo salama la kupitia.

Raia wa Syria waliokataliwa kuondoka eneo la mapigano wanatutia hofu: OCHA

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa una wasiwasi kuhusu hali ya  kibinadamu Kusini Magharibi mwa Syria kutokana na mapigano kupamba moto kwa wiki kadhaa sasa baina ya majeshi ya serikali na  makundi ya wanamgambo yaliyosababisha watu 182,600 kupoteza makazi yao na  wengine 100,000 kukwama katika maeneo ya milima ya Golan na wote wakihitaji misaada.

Katika mkutano na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya binadamu OCHA, Jens Laerke amefafanuahali ilivyo kwa sasa nchini Syria.

(SAUTI YA JENS LAERKE)

“Wakati serikali ya Syria imeweza kuchukua maeneo zaidi katika kipindi cha wiki chache zilizopita, kwa sasa eneo pekee karibu na milima ya Golan ndio bado liko mikononi mwa makundi yenye silaha yasioegemea upande wa serikali, huku eneo la kilomita 200 za mraba kusini mwa nchi hiyo karibu na mpaka wa Jordan liko chini ya  udhibiti wa kundi la Jaysh Khalid Bin Walid Waleed-(JKBW) ambalo lina uhusiano na kundi la ISIL. Umoja wa Mataifa unawasiwasi na vikwazo vilivyowekwa na kundi la JKBW vya kuwazuia raia wanaojaribu kukimbia mapigano.”

Ameongeza kuwa ijapokuwa  idadi kamili ya raia ambao wamekwama katika eneo linalodhibitiwa na JKBW haijulikani, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kabla ya mgogoro  eneo hilo lilikuwa na watu takriban 55,000 na kubaini kuwa tangu wakati huo watu maelfu kadhaa wamefanikiwa kutoroka.

Pia amesema wale waliosalia sasa wanakabiliwa  na uhasama mkali na kati ya 21 na 23 Julai mashambulizi ya angani yaliongezeka katika eneo hilo na watu wengi wanaripotiwa kujeruhiwa.