Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya sitisheni kuwafurusha wakazi wa Kibera si haki:UN

Mtaa wa mabanda wa Kibera, mji kuu, Kenya, Nairobi
Picha ya maktaba ya UM
Mtaa wa mabanda wa Kibera, mji kuu, Kenya, Nairobi

Kenya sitisheni kuwafurusha wakazi wa Kibera si haki:UN

Haki za binadamu

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamelaani hatua ya serikali ya Kenya ya kuwafurusha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Kibera mjini Nairobi na kuitaka serikali kusitisha mara moja zoezi hilo hadi pale hatua za kisheria zitakapokamilika.

 

Kwa mujibu wa wataalamu hao , serikali imepeleka mabulizoda na kubomoa mamia ya nyumba na kusambaratisha takriban shule tano. Operesheni hiyo ya kuwaondoa kwa nguvu wakazi wa Kibera ilianza alfajiri Julai 23 2018 na inatarajiwa kuwaacha watu Zaidi ya 30,000 bila makazi, hivi sasa watoto 2000 wameachwa bila masomo baada ya shule kubomolewa.

Leilani Farha mmoja wa wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki ya nyumba bora anasema “"Uharibifu wa nyumba, shule na mahali pa ibada katika mojawapo ya jamii maskini zaidi nchini Kenya ni kukiuka ahadi zilizofanywa na Serikali ya Kenya kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa au SDGs”

Bomoa bomoa hiyo inafanyika licha ya makubaliano ya awali kati ya mamlaka ya Kenya ya ujenzi wa barabara mijini, tume ya taifa ya ardhi na tume ya Kenya ya haki za binadamu kwamba wataanza mchakato wa kuwalipa fidia  kabla ya kuwafurusha ili kwenda sanjari na misingi ya haki za binadamu.

Bi. Farha ameongeza kuwa zoezi hilo limeanza bila kuwapa tahadhari ya kutosha, na bila mipango yoyote ya wapi pa kuwaweka na malipo yao ya fidia. Wakazi wameshuhudia nyumba zao na shule  zikisambaratishwa kisha wakaanza kuchagura kifusi kuambulia chochote kilichosalimika.

Wengi hawana pa kwenda na wamelazimika kulala katika maeneo ya wazi wakipigwa baridi kali. Amesisitiza kuwa kuwafurusha watu kwa nguvu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuaathiri haki zao za makazi, chakula, maji, afya, elimu na kazi, na kwa kesi hii bomoa bomoa hiyo inakiuka pia uamuazi wa kisheria uliokataza kuwaondoa watu wa Kibera na kuongeza shuku endapo sharia za ardhi za Kenya za kuwalinda watu zilizingatiwa.

Kwa mujibu wa viwango vya sheria za kimataifa watu wote waliotimuliwa kwenye nyumba zao bila kujali wana hati ya umiliki  ama la ni lazima walipwe fidia kwa ajili ya hasara, usumbufu na usafirishaji wa mali zao.

Bomoa bomoa hiyo imefanyika ili kuruhusu ujenzi wa barabara

TAGS: Kenya, Kibera, Haki za binadamu, UN