Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maeneo mapya 24 kujiunga na mtandao wa hifadhi ya urithi wa dunia wa UNESCO

Quirimbas, Msumbiji
UNESCO/hifadhi ya Quirimbas
UNESCO/hifadhi ya Quirimbas, Msumbiji
Quirimbas, Msumbiji

Maeneo mapya 24 kujiunga na mtandao wa hifadhi ya urithi wa dunia wa UNESCO

Masuala ya UM

Baraza la kimataifa la uratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO kuhusu mpango wa binadamu na mazingira, leo limeongeza maeneo mapya 24 kwenye mtandao wa hifadhi ya urithi wa dunia (MAB) katika mkutano unaoendelea mjini Palembang nchini Indonesia.

Mtandao huo sasa una jumla ya maeneo 686 ya hifadhi. Akizungumza wakati wa mkutano huo utakaokunja jamvi Julai 28, mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay amesema “ Kuhifadhi mazingira na udhibiti wa rasilimali za asili katika mfumo wa maisha ni  ni chachu ya maendeleo endelevu," Akiongeza kuwa “Maeneo haya ni maabara ya ushirikiano wa usawa kati ya watu na asili, kuruhusu maendeleo katika sayansi na ujuzi wa jadi. Yanawezesha kushirikiana ujuzi, kuchagiza mahusiano kati ya sayansi na jamii na kusaidia kuleta maboresho halisi kwa maisha ya wakazi wa maeneo hayo, "

Hifadhi ya urithi wa dunia imejumuisha Moldova na Msumbiji kwa mara ya kwanza mwaka huu, huku maeneo  mengine matano kutoka Australia, moja kutoka Uholanzi na lingine kutoka Marekani yameondolewa kwenye orodha hiyo kwa maombi maalumu ya nchi husika.

Miongoni mwa maeneo hayo mapya yaliyoongezwa ni Quirimbas, Msumbiji  lilipo katika jimbo la Cabo Delgado likiwa na visiwa 11 na maarufu kwa utalii, eneo la Arly  lililopo kwenye mbuga ya Savannah nchini Burkina Faso, eneo la Gombe Masito Ugalla nchini Tanzania , eneo ambalo ni kubwa kwa utafiti wa sokwe  (Chimpanzee ), pia linajumuisha mbuga ya taifa ya wanyama ya Gombe, misitu, na sehemu ya ziwa Tanganyika. Pia eneo hilo lina aina mbalimbali za mimea, maua , zaidi ya aina 300 za smaki, zaidi ya aina 250 za ndege, nyoka kama kobra wa majini na nyoka wa ziwa Tanganyika. Nchi zingine ambazo maeneo yake yameingia katika orodha hiyo pia ni Madagascar, Afrika Kusini, Italia, Urusi, Uholanzi, Korea na Ujerumani.

Maeneo ya hifadhi ya urithi wa dunia ni maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya kupatanisha uhifadhi wa viumbe hai na shughuli za binadamu kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za asili.