Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili unaoendelea Cameroon unasikitisha na kuhuzunisha-Zeid

Familia kutoka Cameroon zasaka uhifadhi Utanga, Obanliku nchini Nigeria baada ya kukimbia mzozo katika maeneo kunakozungumzwa kingereza nchini mwao.
UNHCR/Elizabeth Mpimbaza
Familia kutoka Cameroon zasaka uhifadhi Utanga, Obanliku nchini Nigeria baada ya kukimbia mzozo katika maeneo kunakozungumzwa kingereza nchini mwao.

Ukatili unaoendelea Cameroon unasikitisha na kuhuzunisha-Zeid

Haki za binadamu

Serikali ya Cameroon imetakiwa  kufanya uchunguzi huru na wa kina dhidi ya ripoti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vikosi vya usalama na magenge  yenye silaha dhidi ya maeneo ya wazungumzaji wa kiingereza nchini humo.

Wito huo umetolewa leo na kamishna mkuu wa haki za binadamu wa  Umoja wa Mataifa, Zeid  Ra’ad Al Hussein mjini Geneva Uswisi.

Zeid amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na vitendo vya kikatili vinavyoendelea katika sehemu za  Kaskazini, Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon ambako raia wengi ni wazungumzaji wa lugha ya Kiingereza. Miongoni mwa ukatili unaofanywa ni pamoja na mauaji, uchomaji nyumba moto, na utekaji wa watu.

Image
Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’aad al-Hussein. Picha: UN/Jean-Marc Ferré

Hivi karibuni kumetolewa mkanda wa video unaoonyesha  wanajeshi wakimuua mwanamke, mtoto mdogo na mtoto mwingine mchanga kwa Madai kuwa ni wafuasi wa kundi la Boko Haram. Mkanda huo umemghadhibisha Kamisha mkuu na kutaka vitendo hivyo kukomeshwa mara moja.

Zeid ameongeza kuwa, “ kutokana taarifa hizi za ghasia  tumeomba rukhsa ili kuhakikisha madai ya visa hivyo dhidi ya vikosi vya  serikali na magenge yenye silaha lakini hadi sasa hatujaruhusiwa,” hivyo akasema , “ tutatumia njia zingine mbadala kuweza kufuatilia hali hii.”

Duru zinasema, hali iliyoanza kama maandamano mwezi Oktoba  mwaka 2016 katika maeneo ya kaskazini magharibi na pia kusini magharibi dhidi ya ubaguzi, ilibadilka na kuwa ghasia mwaka 2017 na tangu wakati huo hali imekuwa mbaya zaidi .

Kuna taarifa za kutisha zikieleza kuwa magenge yenye silaha yanatekeleza utekaji nyara, kuuwa kwa maksudi mafisa wa polisi na viongozi wa mitaa na pia kuteketeza shule kwa moto, huku duru zingine zikishutumu vikosi vya serikali kuhusika na  mauaji, matumizi ya nguvu kupindukia , uchomaji moto nyumba, kuwakamata watu kiholela na pia kuwatesa.

Umoja wa Mataifa, unasema watu zaidi ya 21,000 wamekimbilia katika nchi jirani kuokoa maisha yao, wengine 160,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani bila makazi na wengi wanadaiwa kujificha misituni.