Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 4000 wapata msaada wa IOM kufuatia mafuriko Burundi

Picha:UM/Sebastian Villar
Wakaazi wa Burundi kama huyu wanapokea msaada kutoka kwa IOM kufuatia mafuriko yanayoshuhudiwa nchini humo.(Picha:UM/Sebastian Villar)

Watu zaidi ya 4000 wapata msaada wa IOM kufuatia mafuriko Burundi

Msaada wa Kibinadamu

Wakazi wa kaya zaidi ya 1000 zilizotawanywa na mafuriko nchini Burundi zipokea msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la wahamiaji, IOM. 

Mafuriko hayo yaliyotokana na mvua kubwa kwenye maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Burundi na maeneo ya mpakani mwa ziwa Tanganyika, yamesambaratisha kabisa kaya zaidi ya 1000 na kuwaacha wakazi wa nyumba zingine 4000 bila makazi huku wakihitaji msaada.

Wakazi hao zaidi ya 4000 ambao wengi wamepoteza kila kitu walilazimika kusaka hifadhi kwa jirani zao, ambao ingawa wamewapa makazi ya muda lakini wanakabiliwa na changamoto za fedha kuweza kumudu mahitaji ya msingi. Maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko hayo ni Nyanza, Gatumba Bujumbura vijijini na maeneo ya milima ya Butere ambako hivi sasa ndiko IOM inatoa msaada.

Kaya 140 zinazohifadhi waathirika zimepokea msaada wa kodi ya pango ya miezi mitatu ili kuwasaidia watu hao wakati wa majira ya kiangazi ambapo ajira katika sekata ya kilimo inakuwa ngumu, Stephanie Vavyarinana ni miongoni mwa wafaidika anasema “Mafuriko yalipozuka nyumba yangu ilisambaratishwa kabisa na nilipatwa na taharuki, tunakaribisa msaada huu wa IOM, kwani ukipata watu wa kukusaidia unachoweza kufanya ni kushukuru.”

Mbali ya fedha msaada mwingine wanaopewa ni madumu ya kuhifadhi maji, ndoo, vyombo vya kupikia, magodoro, mablanketi, kilo mbili na nusu za sabuni na shirika la afya ulimwenguni WHO likatoa vyandarua vya mbu, 597 vilivyo na dawa.

Vifaa vyote hivyo vimepatikana kwa ushirikiano wa IOM na ofisi ya Marekani inayohusika na msaada wa nje wa majanga USAID, Idara ya maendeleo ya kimataifa ya Uingereza, chama cha msalama mwekundu nchini Burundi, na watu wa kujitolea .

TAGS:Burundi, IOM, USAID, Mafuriko,