Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utaratibu wa Israel unaenda kinyume na sheria za haki za kimataifa:Zeid

Kijana akitazama mandhari ya Jabalia kambi kubwa kabisa kati ya kambi 8 za a wakimbizi Ukanda wa Gaza . Ipo Kaskazini mwa Gaza karibu na kijiji cha Jabalia.
Picha na Suhair Karam/IRIN
Kijana akitazama mandhari ya Jabalia kambi kubwa kabisa kati ya kambi 8 za a wakimbizi Ukanda wa Gaza . Ipo Kaskazini mwa Gaza karibu na kijiji cha Jabalia.

Utaratibu wa Israel unaenda kinyume na sheria za haki za kimataifa:Zeid

Amani na Usalama

Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein amesema   kumekuwa na uchunguzi mdogo sana dhidi ya vikosi vya ulinzi vya Israel ambavyo vinatekeleza ukatili dhidi ya Wapalestina na hata unapofanyika hauna nguvu dhidi ya washutumiwa kuweza  kuchukuliwa hatua za kinidhamu na hukumu ikitolewa  huwa ni ndogo ikilinganishwa na makosa yaliyofanywa.

Akizungumza kwenye mkutano wa kamati ya haki za msingi za watu wa Palestina kwa njia ya video hii leo kutoka Geneva Uswisi , kamishna Zeid amesema

(SAUTI YA ZEID AL HUSSEIN)

 “ Licha ya Israel kuweka uratibu kadhaa  wa uwajibikaji kuna wasiwasi mkubwa  kuwa uratibu huo   hauendani na viwango huru vya kimataifa , visivyo na upendeleo na vyenye kuzaa matunda yaliyotarajiwa.”

 Na kuhusu hatua ya bunge la Israel ya hivi majuzi kupitisha sheria mpya ya utaifa amesema

(SAUTI YA ZEID AL HUSSEIN)

 “Wiki iliyopita Israel ilipitisha sheria kuhusu utaifa, ambayo ni ya ubaguzi dhidi ya jamii zisizo za kiyahudi, hususan raia wa Israel wenye asili ya kiarab pamoja na wale wanaoishi katika eneo la Jerusalem linalokaliwa  sheria ambayo yaweza pia kuchochea ghasia zaidi.”

Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza
OCHA
Hospitali ya Ash Shifa mjini Gaza

 

 Naye balozi wa Palestina Riyad Mansoor kuhusu suala hilo amesema huko ni kuweka sheria  inayotoa upendeleo na kutoa  haki maalum kwa watu wa itikadi fulani dhidi ya wengine wenye uraia na itikadi tofauti hivyo

(SAUTI YA RIYAD MANSOUR)

Ni sheria ya kibaguzi na ni kipengee kingine cha kuelekea katika ubaguzi wa rangi au apartheid.”

Tarehe 30 Machi mwaka huu, wapalestina katika ukanda wa Gaza ambao unadhibitiwa na  kundi la Hamas, walianza maandamano kupinga  vizuizi ambavyo vimewekwa  na Israel tangu mapema mwaka 1990.

Na uhasama baina ya pande hizo mbili, Israel na Palestina umezidi kuchacha. Na tangu Jumatatu iliyopita , wakuu wa Israel  walizuia kuingizwa  mafuta katika sehemu za Gaza kama sehemu ya kuzidisha makali ya kuzuia bidhaa kutoka nje kuingia katika eneo hilo. Israel inasema inafanya hivyo kufuatia urushaji wa tiara kutoka Gaza hadi Israel ambazo zimesababisha uharibifu.

Bunge la Israel lilipitisha sheria  hiyo kwa kura 62 za ndio na 55 za kupinga huku wawili hawakupiga kura kabisa, sheria inayoeleza kwamba Israel ni taifa la Waisrael na si vinginevyo.