Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaalani shambulio dhidi ya ofisi zake Bunj Sudan Kusini

Mlinda amani anayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio
UNMISS
Mlinda amani anayehudumu nchini Sudan Kusini akihudumia mwanamke mjamzito anayeugua malaria.Watoa huduma wakati mwingi ni walengwa wa mashamubulio

UNHCR yaalani shambulio dhidi ya ofisi zake Bunj Sudan Kusini

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, leo limelaani vikali shambulio dhidi ya ofisi zake kwenye mji wa Bunj Kaskazini Magharibi mwa Sudan Kusini, ambalo limejeruhi wafanyakazi wawili wa Umoja wa Mataifa.

Mapema leo asubuhi UNHCR iliarifiwa kuhusu maandamano katika eneo hilo yanayodai fursa za ajira kwa jamii za wenyeji. Waandamanaji waliingia kwa nguvu kwenye ofisi za UNHCR na kupora katika ofisi hizo na makazi ya wafanyakazi wa UNHCR.

Kwa mujibu wa shirika hilo maskani mengine ya mashirika 10 pamoja na ofisi ya tume ya masuala ya wakimbizi vilishambuliwa na kuporwa.

UNHCR imeiomba mamlaka kuhakikisha usalama na ulinzi kwa wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu.

Shirika hilo linaendelea kushirikiana na uongozi wa eneo hilo na wawakilishi wa jamii zinazowahifadhi ili kurejesha hali ya kawaida.

Walinda amani wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS walipelekwa mara moja katika eneo la Bunj ili kurejesha utulivu na kuyasaidia mashirika ya misaada ya kibinadamu.

TAGS: UNHCR, Bunj, Sudan Kusini, UNMISS, uporaji