Wakimbizi wenye matatizo ya figo Jordan nyota ya jaha yawaangazia
Wakimbizi wa Syria takriban 171 wanaoishi nchini Jordan wamekuwa wanasumbuliwa na matatizo ya figo na tiba yake ni gharama kubwa wasiyoweza kuimudu hadi sasa ambapo habari njema imewaletea matumaini mapya.
Wakimbizi hao ambao wengi ni masikini na hata mlo wao ni lazima wapewe msaada , walianza kupoteza matumaini kwani kama hawawezi kumudu kununua chakula watawezaje kumutu tiba ya dola 11,000
Ndipo mfuko wa usaidizi wa kibinadamu wa Jordan (JHF) ukaingilia kati kunusuru maisha yao. Baada ya kuanza kupoteza matumaini ikizingatiwa kwamba watu hao ni wakimbizi hivi sasa wanapata matibabu ya bure kwa hisani ya mfuko huo.
Miongoni mwao ni Fayzeh Faeq Zardan, huku machozi yakimlengalenga anasema peremende tu ya mwanangu ni mtihani sembuse dawa “nimemwambia mtoto wangu wa kiume wa miaka mitatu kwamba HAPANA kwamba hatapata peremende …hatuwezi kumudu kuzinunua.”
Vita vinavyoendelea Syria kwa mwaka w asaba sasa vimewafanya watu zaidi ya laki sita kukimbilia Jordan tangu 2014 na asilimia kubwa wanapatiwa msaada namfuko huo wa usaidizi wa Jordan.
Zardan mwenye umri wa miaka 38 ni mkimbizi kutoka mji wa magharibi mwa Syria wa Homs naye ni mgonjwa wa figo.“Sina hata pesa za kulisha familia yangu au za kugharimia sindano hii,’ amesema huku akionyesha mashine ilioko kwenye mkono wake.
Mashine hiyo humsaidia mgonjwa wa figo kutoa uchafu pamoja na chumvi ya ziada mwilini na majimaji kutoka kwenye damu ilikuwezesha figo kufanya kazi.
Mbali na mashine hiyo pia kwa kipindi cha miaka mitatu amekuwa akipata sindano za kila wiki kutoka katika zahanati ya chama cha mwezi mwekundu cha Jordan.
Mita chache kutoka kitanda chake ni mgonjwa mwingine Ghassan Nader Al Barq mwenye umri wa miaka 51. Alianza shida ya figo akiwa Syria miaka minane iliyopita , na alikimbilia Jordan miaka sita iliyopita na akapata tiba ndogo katika hospital ya binafsi mjini Amman lakini gharama zilikuwa juu akashindwa kumudu.
Kati ya wakimbizi hao 171 kutoka Syria walio na matatizo ya figo 124 kati yao wanapata matibabu kupitia mfuko wa JHF, ilhali 37 wanatibiwa kupitia msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, na 10 kupitia asasi mbalimbali za kiraia.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2016 ya wizara ya afya ya Jordan, gharama ya kutibu figo ni kwa wastani wa dola 11,000 kwa kila mgonjwa na asilimia 93 ya wakimbizi walioko Jordan hawawezi kumudu.