Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumuishaji wakimbizi Ureno waleta nuru mashambani

Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea
Frontex/Francesco Malavolta
Wasaka hifadhi wakiokolewa na meli ya ubelgiji katika bahari ya mediteranea

Ujumuishaji wakimbizi Ureno waleta nuru mashambani

Wahamiaji na Wakimbizi

Mradi wa mfano wa kuvutia  uwekezaji na nguvu kazi nchini Ureno hivi sasa unajumuisha wakimbizi wanaowasili nchini humo kupitia mpango wa Muungano wa Ulaya wa kuwapatia makazi mapya wakimbizi.

Ni katika mji mdogo wa Idanha-a-Nova katikati mwa Ureno ambako mradi huo wa mfano unatekelezwa. Sauti  za ndege zikiashiria eneo hili la mashambani huku vijana wawili Bashir na Said wanaonekana wakifanya kazi.

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa ugatuzi wa serikali ya Ureno wa kulenga kufufua maeneo ya mashambani yenye idadi ndogo ya watu baada ya vijana kukimbilia mijini. 

Said na Bashir wamekuwepo hapa kwa miezi sita baada ya kutoroka Eritrea na kufunga safari ndefu iliyowapitisha maeneo kadhaa ya bara lao la Afrika  wakitafuta usalama. Said anasimulia..

(SAUTI YA SAID)
“Nina bahati. Marafiki zangu wengi walizama baharini wakiwa njiani kwenda Italia kupitia Libya au Misri. Walizama katikati ya bahari na mimi ni na bahati.”

Kupitia mradi huu wa kilimo unaowezesha watu kupata  haraka ajira na nyumba, manispaa inatarajia kudhihirisha kuwa maeneo ya mashambani yana uwezo wa kushindana na maeneo ya mijini.  Pedro Guerra ni meneja wa kituo hiki.

“Tunawaajiri wakimbizi kwa sababu tuko katika eneo lenye rutuba na uzalishaji mwingi lakini idadi ya watu ni wachache. kwa hivyo tunahitaji watu zaidi ili kusaidia eneo letu kupata maendeleo. Pia ni nafasi nzuri kwetu na kwao pia.”

Said amepata kibali cha kazi na punde ataanza kazi mpya ya afisa uhusiano wa manispaa ambapo atasaidia kuimarisha uhusiano  kati ya eneo la Idanha na wageni…

“ Naweza kuwapa ushauri kutokana na uzoefu wangu wa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu.Si rahisi kuishi Ureno, lakini baada ya muda mambo hubadilika siku baada ya siku. Ni lazima uwe mvumilivu kuweza kufikia lengo lako.”

Mwaka jana Waziri Mkuu wa Ureno alitangaza kufanya kipaumbele chake suala la kukaribisha nchini mwake wakimbizi kutoka Uturuki na maeneo mengine ya nchi ya tatu walikohamishiwa.